Dar es Salaam. Alianza kama mwalimu wa kawaida, akaibuka kuwa mmoja wa mawaziri walioteka hisia za wengi kwa namna yake ya uongozi na misimamo isiyotetereka.
Alikuwa mtoto wa kijiji cha Mapogoro kabla ya kuwa mtu wa Dodoma. Huyo ndiye William Vangimembe Lukuvi jina lililojijenga taratibu hadi kuwa alama ya uzoefu katika siasa za Tanzania sambamba na uongozi.
Hata hivyo, hakuna anayezungumza na Mungu, ikafika Saa moja asubuhi leo Jumatano, Machi 25, 2026, safari yake hapa duniani imefikia tamati. Moyo wake umesimama akiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, akiacha pengo ambalo hata wakosoaji wake wanaweza kukiri si rahisi kuliziba.
Mtoto wa udongo wa Mapogoro
Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955, katika Kijiji cha Mapogoro, wilayani Iringa Vijijini, inaweza kuelezwa kwamba ndoto kubwa mara nyingi huzaliwa kimyakimya.
Hakukuwa na ishara kwamba mtoto huyo angekuja kusimama mbele ya viongozi wakuu wa nchi na kushika nyadhifa nyeti serikalini.
Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Kitanewa kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu Tabora mwaka 1975. Hapo ndipo alipoanza safari yake ya ualimu, kazi aliyoifanya kwa moyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 1975 hadi 1980 chini ya Wizara ya Elimu.
Hata hivyo, ndani yake kulikuwa na msukumo uliomvuta zaidi ya darasa. Alitamani kushiriki katika uamuzi mpana unaogusa jamii kwa ujumla.
Kutoka Moscow hadi Washington
Hata hivyo, miaka ya 1980 ilimkuta Lukuvi akiwa mbali na nyumbani, alikuwa katika mji wa Moscow, kitovu cha mijadala mikali ya kisiasa wakati huo.
Akiwa katika Chuo cha Komsomol kati ya mwaka 1982 na 1983, alikopata Diploma ya Sayansi za Siasa.
Huko hakujifunza tu nadharia za vitabuni, bali alijenga upeo kupitia mijadala na wanafunzi kutoka mabara mbalimbali. Uzoefu huo ulimjengea Lukuvi msingi wa uongozi aliokuja kuudhihirisha baadaye.
Miaka mingi baadaye, akiwa tayari kiongozi mwenye uzoefu, alirejea masomoni na kupata Shahada ya Kwanza katika masomo ya Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Washington na kisha Shahada ya Uzamili katika Sayansi za Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Tasnifu yake ya uzamili iliyochambua changamoto za demokrasia na utulivu wa kisiasa nchini, ilimuonyesha Lukuvi namna alivyotafakari siasa si tu kama mshiriki, bali pia kama mtafiti.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ulioashiria mwanzo wa mfumo wa vyama vingi, Lukuvi aliingia katika ulingo wa siasa kwa kuwania Jimbo la Isimani. Wananchi walimpa ridhaa.
Kuanzia hapo, hakutazama nyuma. Kwa kipindi cha miaka 30 ameendelea kushinda uchaguzi mara sita mfululizo, jambo linalomweka miongoni mwa wabunge waliodumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Bunge la Tanzania.
Uwezo wake wa kusimama imara katika nyakati za kisiasa zenye misukosuko ulimfanya kuheshimika hata na wachambuzi wa siasa waliomwona kama hazina ya uzoefu isiyopatikana kirahisi.
Mwaka 2015, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli, alimpa dhamana ya kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara yenye changamoto kubwa kutokana na migogoro ya ardhi.
Katika kipindi chake, alisimamia utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya milioni mbili, hatua iliyowawezesha wananchi wengi kumiliki rasmi mali zao na kuzitumia kama dhamana ya kiuchumi.
Lakini pengine tukio lililoonyesha zaidi msimamo wake lilitokea mwaka 2017. Nyumba yake mwenyewe, iliyokuwa katika eneo la hifadhi ya barabara, ilipaswa kubomolewa.
Badala ya kutumia madaraka yake kuizuia, aliacha sheria ichukue mkondo wake. Wakala wa Barabara Tanzania (Tamroads) walibomoa nyumba hiyo na waziri akabaki kuwa mfano wa utii wa sheria.
Mwaka 2018, alifanya ziara katika wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera, ambako alikutana na mamia ya wananchi kila siku, akisikiliza kero zao moja kwa moja. Alijijengea taswira ya kiongozi anayesikiliza, anayekaa karibu na wananchi na anayechukua hatua.
Lakini Mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alimwondoa katika Wizara ya Ardhi kwa heshima, akieleza umuhimu wa uzoefu wake katika kusaidia kizazi kipya cha viongozi.
Baadaye, aliteuliwa kuwa Mshauri Maalumu wa Rais kabla ya kurejea serikalini mwaka 2024 kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), nafasi aliyoiendelea kushika hata baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Kama ilivyo kwa viongozi wengi wa kisiasa, hakukosa ukosoaji. Baadhi ya sera zake zilikumbana na upinzani na kulikuwa na mjadala kuhusu baadhi ya masuala yake binafsi na kisiasa. Hata hivyo, mchango wake unabaki kuwa sehemu ya historia ya uongozi nchini.
Anakumbukwa kama mwalimu aliyekuwa waziri, mbunge wa muda mrefu na kiongozi aliyethubutu kuweka sheria mbele hata pale ilipomgusa binafsi.
Safari yake hapa duniani imetamatika kimyakimya kama ilivyoanza. Lakini habari za kifo chake zimesambaa kwa kasi, zikigusa hisia za wengi kutoka Isimani hadi Kagera na kutoka bungeni hadi mitaani.
Tanzania imepoteza mmoja wa wanasiasa wake waliobeba uzoefu wa miongo kadhaa, urithi ambao utaendelea kujadiliwa kwa miaka mingi ijayo.
