Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amesema Ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB), katika miradi ya kimkakati unaendelea kuimarika jambo linawezesha nchi kukua kiuchumi.
Ameyasema hayo Machi 25, 2026 alipokuwa anapokea nakala za hati za utambulisho za Mwakilishi Mkazi mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania Bi. Mary Manneko Monyau, katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kombo amesema miradi hiyo imejikita zaidi katika sekta za miundombinu, usafirishaji, na nishati ambazo ni uti wa mgongo wa mabadiliko ya kiuchumi nchini. Ameongeza kuwa kwa sasa Benki hiyo inafadhili miradi 27 ikiwemo Barabara ya Mzunguko wa Nje ya Dodoma, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa nyaya za umeme za chini ya bahari unaounganisha visiwa vya Zanzibar, Pemba, na Mafia.
Aidha amempongeza Bi. Monyau kwa uteuzi wake na kueleza kuwa Serikali ina imani kubwa na uzoefu wake, hususan kutokana na mafanikio aliyoyaonesha alipokuwa Mwakilishi Mkazi nchini Sudan.
Kwa Upande wake Bi. Monyau amesisitiza kuwa AfDB itajikita zaidi katika kuoanisha mipango yake na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 ambapo imepania kuongeza upatikanaji wa mitaji na kusaidia miradi inayoinua uhuru wa kifedha wa Tanzania, huku ikizingatia kukuza ajira kwa vijana na miundombinu wezeshi itakayochochea ukuaji wa viwanda na biashara kanda nzima.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


