Lukuvi umeitwa marehemu, oh! Mnyalukolo, Vahungilage…

Dodoma. Gwiji wa muziki Ramadhan Mtoro Ongala (Dk Remmy) aliwahi kuimba wimbo wake kuwa ‘kifo hakina huruma.’

Katika moja ya vitabu vitakatifu kimeandika, kilio kilisikika Rama, Rahel akiwalilia watoto wake asikubali kufarijiwa kwa kuwa hawapo tena na ndivyo ilivyo, kilio kimesikika Dodoma, Rais akimlilia waziri wake kwa kuwa hayupo.

Kwenye wimbo huo ametaja mambo kadhaa lakini leo tuondoke na hili kwamba kifo hakina huruma. Basi huku bungeni ndiyo kama mlivyosikia kwamba nguzo imeanguka.

Ni mwamba kutoka Isimani, Mkoa wa Iringa, Jimbo ambalo unaweza kusema limekuwa na matukio ya aina yake, kwanza kwa mbunge wake kuhudumu miaka 31 bungeni si mchezo lakini ndiyo kwa akina Said Mwamwindi na Dk Kleruu.

Lukuvi (Nimwite marehemu sasa) moja ya mambo ya kukumbukwa ni namna alivyofanya kazi na maspika sita mfululizo akiwemo Pius Msekwa, Samwel Sita, Anne Makinda, Job Ndugai, Dk Tulia Ackson na Mussa Zungu. He! Kumbe alidumu.

Rest In Peace mwamba William Vangimembe Lukuvi, japo kuna mapungufu ya ubinadamu lakini hukuwa na baya kwa Wana-Isimani ndiyo maana walikurudisha kila mwaka.

Huyu ni miongoni mwa wabunge walioingia kwenye rekodi za kukaa muda mrefu bungeni akiwemo Dk Christian Mzindakaya na Anne Makinda. Daaa mwacheni Mungu aitwe Mungu maana kazi yake haina makosa.

We vuta hisia kwamba, zile suti kali za mtu anayetoka jengo la utawala asiye na tabia ya kubeba mkoba badala yake anabeba simu ya bei ndefu mkononi lakini hatuwezi kumwona tena.

Sauti ya mvumo wa kutengua kanuni za Bunge kwenye matukio, majibu ya kejeli kwa wabunge wa upinzani lakini yasiyokwaza ndiyo haipo tena bungeni.

Masikini Lukuvi, lala salama mtu uliyeweka rekodi za kuzunguka kwenye wizara na kote ukaandika historia, lakini kumbukumbu nzuri ya wewe kusimamia uchaguzi wa maspika watatu katika chaguzi za mfululizo.

Lukuvi huko uendako msalimie Job Ndugai, mkumbushe kuwa ulisimamia uchaguzi wake akikalia kiti cha Spika, mwambie huku wanapokuwa manaibu ndiyo wanakuwa maspika na sasa yupo rafiki yake mkubwa Mussa Zungu mwana-Simba mwenzake.

Hivi watu wanajua kuwa Novemba 11, 2025 ulisimamia uchaguzi wa Spika Zungu alipopindua meza na kumuacha Dk Tulia Ackson ambaye naye ulisimamia uchaguzi wake pale mbele.

Sauti yako ilisikika uliposema pale mbele ya kiti cha enzi cha Bunge wakati unaongoza uchaguzi wa Zungu …“ikugombea uspika kwani nilijua ningekuwa Spika” oh Mnyalukolo, Vahungilage (wasalimie).

Sina uhakika kama wabunge waliwahi kukuomba siri ya kukaa muda mrefu mjengoni maana wengi hutamani lakini hawafikii viwango hivyo. Miaka 31 mjengoni ni zaidi ya umri kwa wabunge wengi waliopo sasa.

Mwamba kutoka ubunge, ukuu wa Mkoa Dodoma na Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Vijana, Waziri wa Ardhi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Ajira na Wenye Ulemavu kwa vipindi tofauti lakini eti leo umeitwa marehemu.

Angekuwepo bungeni Halima Mdee angeweza kusimulia hasa kile kidole alichokuwa akimnyooshea huku akionyesha tabasamu la utani.

Ni katika kipindi ambacho Tundu Lissu alipokuwa mjengoni walikuwa wakipeana vijembe lakini wakitoka Lukuvi alimfuata na kushikana mikono.

Haya sasa, twendeni tukamwombolezee William Lukuvi miaka 70 aliyoishi duniani ndiyo mwisho wa enzi yake na sote tutakwenda katika safari hii aliyoiendea.

Mwili wa Mwana-Isman huyu utazikwa Jumanne ya Machi 31, 2026, kijijini kwao Idodi, mkoani Iringa.