Pretoria. Mamlaka kupambana na rushwa nchini Afrika Kusini imewakamata maofisa 12 waandamizi wa polisi kwa tuhuma za rushwa na udanganyifu.
Maofisa hao walifikishwa mahakamani jana Jumatano Machi 25, 2026 katika mji mkuu, Pretoria.
Miongoni mwa watuhumiwa hao yupo, Kamishna wa Kitaifa wa Polisi, Fannie Masemola ambaye amekabidhiwa hati ya kumtaka afike mahakamani mwezi ujao kuhusiana na uchunguzi wa mkataba unaodaiwa kuwa wa kifisadi wa kutoa huduma za afya na ustawi kwa maofisa wa polisi.
Uchunguzi huo imeelezwa awali, uliagizwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye pia alimsimamisha kazi waziri anayeshughulikia masuala ya polisi mwaka jana.
Msemaji wa Polisi, Athlenda Mathe ametoa taarifa hiyo jana wakati wa kesi ya maofisa hao wakifikishwa mahakamani.
Kukamatwa kwao kunatokana na uchunguzi unaendelea kuhusu madai ya rushwa katika ngazi za juu ndani ya Jeshi la Polisi la Afrika Kusini.
Uchunguzi mwingine wa pili unaoendeshwa na Bunge pia unachunguza madai kwamba baadhi ya maofisa waandamizi wa polisi walikuwa na uhusiano wa kifisadi na wanaodaiwa kuwa wakuu wa uhalifu, na katika baadhi ya matukio walipokea fedha kutoka kwao kwa ajili ya upendeleo maalumu.
Kukamatwa kwa maofisa hao 12 kunahusiana na mkataba unaodaiwa kuwa wa kifisadi wa kutoa huduma za afya na ustawi kwa maofisa wa polisi, kwa mujibu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Rushwa cha Mamlaka ya Taifa ya Mashtaka.
Maofisa hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza jana Jumatano pamoja na Vusimuzi Matlala ambaye ni mmiliki wa kampuni iliyopata zabuni ya kutoa huduma kwa jeshi hilo.
Maofisa wote waliwasilisha hati za kiapo kuunga mkono maombi yao ya dhamana na waendesha mashtaka waliieleza Mahakama ya Hakimu ya Pretoria kwamba hawatapinga dhamana yao.
Baadhi ya maofisa hao waliokamatwa walikuwa miongoni mwa wanakamati wa zabuni iliyotathmini na kutoa zabuni hiyo.
