Wanafunzi wawili wanusurika kufa maji Mto Lwiche, mmoja akitafutwa

Rukwa. Watoto watatu wamenusurika kufa maji katika Mto Lwiche uliopo katika Kijiji cha Kasisiwe, Kata ya Milanzi, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo mmoja bado hajapatikana hadi sasa.

Tukio hilo limetokea jana Machi 25,2026 saa 11 jioni wakati wanafunzi hao wakirejea nyumbani kutoka shuleni, ambapo walizama majini.

Watoto wawili wameokolewa na wako salama huku mmoja anayetambulika kwa jina la Huruma Isaack akiendelea kutafutwa na hadi sasa juhudi za uokozi zinaendelea.

Mkazi wa eneo hilo, Getruda Maufi ameeleza masikitiko yake na kuomba kujengewa shule ya sekondari ndani ya kata yao, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza hatari kwa wanafunzi kulazimika kuvuka maeneo hatarishi wanapokwenda kusoma katika shule za kata jirani.

Naye, Conrad Chekwe amesema kivuko kilichopo sio salama ni hatarishi kwa wananchi hususani katika kipindi hiki cha masika, ambapo ameitaka Serikali kuweka mikakati thabiti itakayodhibiti changamoto hiyo.

β€œTukio hili si la kwanza, changamoto ipo muda mrefu, tunaomba viongozi wetu watuwekee kivuko imara ili kupunguza majanga kama haya yasijirudie tena,” amesema Chekwe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kasisiwe, Ezekiel Mwakasege amesema zipo hatua za awali ambazo walichukua ikiwemo kutoruhusu watoto kupita katika maeneo hayo, lakini walifikisha taarifa kwa mamlaka husika ili kuona namna ya kujenga daraja.

Akizungumza wakati wa shughuli za uokoaji, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile amewataka wazazi na wananchi kwa ujumla kuhakikisha watoto wanatumia njia salama, hususan barabara kuu, badala ya kupita katika maeneo ya mtoni ambayo si salama.