Watengeneza maudhui nchini wapewa elimu ya fedha

Dar es Salaam. Wakati tasnia ya uzalishaji maudhui mtandaoni ikizidi kushika kasi nchini, watengeneza maudhui hao (content creators) wametakiwa kuzingatia matumizi ya fedha, kuweka akiba, kusimamia miradi yao, pamoja na elimu ya uwekezaji.

Sambamba na hilo wametakiwa kuzingatia ulinzi wa taarifa binafsi wakati wa kuandaa maudhui yao, lugha za kigeni ili wauze nje, bila kusahau kuzingatia maadili ya Kitanzania.

Hayo yamebinishwa leo Machi 26, 2026 wakati wa mafunzo kwa watengeneza maudhui yaliyoandaliwa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ulio chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB. Mafunzo hayo yamefanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Nyakaho Mahemba amesema kundi hilo limepewa elimu ikiwa ni sehemu ya kuinua ubora wa kazi za sanaa, kujiendesha kibiashara pamoja na kuzalisha ajira zaidi.

Amesema hadi sasa watengeza maudhui 3,191 wamejisajili kikamilifu na kuingizwa katika kanzidata ya wizara ambapo 1697 wanaume 1,158 wanawake.

Hatua ya kujisajili inakuja baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kusema wizara imepatiwa Sh2 bilioni itakayowawezesha watengenezaji wa maudhui mbalimbali mitandaoni kuimarisha kazi zao na kuwaongezea kipato kupitia majukwaa ya kidijitali.

Makonda alibainisha hayo Januari 29, 2026 jijini Dodoma ambapo alisema fedha hizo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuyawezesha makundi yote ya watengeneza maudhui ikiwemo katika sekta ya utalii, michezo, habari, jamii, muziki, filamu na sanaa nyinginezo.

Akifafanua zaidi, Mahemba amesema tayari maombi 137 ya mikopo yenye thamani ya Sh3 bilioni yamewasilishwa kwenye mfuko na tayari umetoa mikopo ya Sh555 milioniΒ  kwa watengeneza maudhui watano ambapo mwanamke ni mmoja aliyepata Sh200 milioni na kampuni nne.

β€œNitoe rai kwa kundi hili wanatakiwa wajaze fomu, zichakatwe waingiziwe hela wakafanye kazi ila kikubwa warejeshe mikopo kwa wakati na wadau wengine waweze kunufaika,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Emmanuel Ndumukwa amesema kundi hilo la vijana linazidi kukua kila kukicha hivyo wanatakiwa wasajiliwe kwenye bodi ya filamu ambapo itawapatia ithibati ya kupata mikopo.

Conrad Coy, maarufu Coy Mzungu amesema elimu ya kifedha kwa watengeneza maudhui itawafanya wafanye kazi zao kwa ubora sambamba na kuweza kukopesheka.

“Mafunzo haya yamefungua mlango ya uelewa wa kifedha kwa vijana wetu hasa kwenye uelewa wa jinsi ya kupata na kuongeza mapato kupitia uzalishaji maudhui,” amesema.

Neyla Manga amesema ni jambo la msingi kwa mtengeneza maudhui kujua namna ya kuzalisha fedha kupitia kazi zake hizo jambo ambalo litawasaidia wengi.

“Nikifahamu namna ya kuzalisha fedha, nikikopa nitakua najua nafanya maudhui yanayoweza kuzalisha pesa kwakuwa natumia vifaa vya gharama kwa hiyo naweza kujua nikifanya kitu fulani kitaweza kunirudishia gharama zangu,” amesema Neyla.

Kwa upande wake, Dk Raphael Mallaba amesema bima zinaweza kumsaidia mtengeneza maudhui ikiwa pamoja na kumlinda kifedha.

“Leo hii akiugua na hana bima anaweza akaingia mfukoni akatumia pesa nyingi. Akiwa na bima kama ya afya anaweza kusaidiwa na kusimama na akaendelea,” amesema.

Jambo la kufanya amesema kampuni za bima mbalimbali kama afya na maisha, magari zinaweza kuungana na na watengeneza maudhui na kupata fedha kupitia matangazo.