SMZ yapigia chapuo matumizi ya teknolojia katika uvuvi

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema inaendelea kutekeleza kwa vitendo sera ya uchumi wa buluu hususani kuongeza thamani ya mazao ya baharini ili kuimarisha kipato kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mboja Ramadhan Mshenga ametoa kauli hiyo leo Machi 26, 2026 wakati akifungua jukwaa la uvuvi Zanzibar, akisema sekta hiyo imetoa ajira zaidi ya 100,000.

Katika ajira hizo, asilimia 17 ni wanawake pekee, hivyo kuna kila sababu kwa Serikali kutafuta namna bora ya kutekeleza uvuvi endelevu.

“Dhana ya uchumi wa buluu inazidi kutekelezwa kwa vitendo kuchochea uzalishaji na rasilimali za bahari,” amesema.

Amesema kwa dunia ya sasa, matumizi ya teknolojia yana nafasi kubwa katika kufanikisha uvuvi salama wa kimazingira na ulinzi wa viumbe bahari kwa kuweka mipango maalumu ya matumizi kupitia teknolojia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Hamad Bakari Hamad ametoa wito kwa wavuvi kujitokeza kwenye sensa itakayofanywa ili kupatikana idadi halisi itakayosaidia kupata huduma zilizopewa kipaumbele na kueleza vikwazo vinavyowakabili katika kazi zao.

Naye, Mkurugenzi Idara ya Uhifadhi wa Bahari Zanzibar, Dk Makame Omar Makame amesema maendeleo ya uvuvi na uchumi wa buluu, yanategemea sekta ya bahari kwa kutunza mazingira na kuhifadhi bahari.

Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wavuvi kutumia njia bora za uvuvi zisizoharibu mazingira ikiwemo kutumia mitego inayokubalika.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari Zanzibar, Dk Zakaria Ali Khamis amewasihi wavuvi kubadilika kutokana dunia ya sasa inayokimbia na teknolojia kutumia vifaa kama Fishfinder GPS ili kuvua kwa tija na masilahi nchini.

“Wavuvi hatuna budi kubadilika, dunia ya sasa inakimbia lazima na sisi tukimbie nayo katika matumizi ya teknolojia,” amesema.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar, Mussa Ramadhan Said amesema ajira mbalimbali hapa nchini zimetokana na shughuli za uvuvi, hivyo hakuna budi kuendelezwa jukwaa hilo kwa ajili ya kupata uzoefu kwa wavuvi na utaalamu wa kisasa kwa wataalamu wa uvuvi.

Kwa upande wao, maofisa na wavuvi wameeleza namna uhifadhi wa bahari na kukomesha uvuvi haramu unavyosaidia kuimarika shughuli hizo kisiwani humo.

Ofisa wa uvuvi, Sharifa Mohammed Miraji ameeleza changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya uvuvi na ufugaji yakiwemo mabadiliko ya tabianchi na uvuvi haramu akisema hakuna budi kwa wavuvi kufuata maelekezo ya wataalamu ili kwenda sambamba na sera za nchi.

Ali Mwalim Mahafoudh amesema kwa kiasi kikubwa rasilimali za eneo la Uroa zimeimarika kutokana na wavuvi wenyewe kuwa tayari kuachana na uvuvi haramu kulinganisha na maeneo mengine ya Hifadhi ya Ghuba ya Chakwa ya Zanzibar.

Zahor Maalim amesema ili uvuvi uwe endelevu lazima wavuvi waendane na uvuvi wa kisasa kwa maslahi ya sasa na kizazi cha baadaye.

Mdau wa uvuvi, Dk Narriman Jidawi amesema kuwepo kwa jumuiya ya wanawake wavuvi kumeleta  mwamko mkubwa wa ajira  kwa vijana kutokana na ongezeko la mnyororo wa thamani ya biashara ya dagaa na uchakataji wa mwani kwa wanawake wa Zanzibar.

Jukwaa hilo lenye kaulimbiu “Matumizi ya Teknolojia kwa Uvuvi wa Kisasa na Salama”, linalenga kuhamasisha teknolojia kutumika zaidi katika shughuli za uvuvi.