WIZARA ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, imeingia mkataba wa miaka 15 na kampuni ya Bahari Leisure kwa ajili ya kuendesha Viwanja vya Wilaya na Mkoa vilivyopo Unguja na Pemba.
Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Ali Abdulgulam Hussein amesema lengo la kufanya makabidhiano hayo ni kuendesha na kusimamia viwanja hivyo.
“Wizara imeamua kufanya makubaliano hayo, kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Uwekezaji ili viweze kuendeshwa kwa ufanisi kwa kuvitunza na kuleta tija kwa taifa,” amesema.
Pia, amesema uwekezaji huo umetoa fursa kwa jamii na watu wenye uhitaji maalumu ambao walikuwa wanatumia kiwanja hicho kabla ya kujengwa jambo ambalo litakuza vipaji na kutoa mafunzo kwao.
Naye, Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame, amewataka wananchi kushirikiana na muwekezaji ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.
Vilevile, amewataka wadau wa michezo nchini kushirikiana na Taasisi ya Bahari Leisure ili viwanja hivyo viweze kutumika kwa ufanisi na kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bahari Leisure, Ibrahimshah Faisal Shahbhai, amehidi kuyatekeleza makubaliano hayo kuondosha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Makubaliano hayo yamefanyika kwenye Uwanja wa Maisara uliopo Wilaya ya Mjini ambapo yameshuhudiwa na Naibu Waziri na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Uwezeshaji na viongozi wengine.
