*********
WAZIRI Mstaafu wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Wanawake Amani na Usalama kupitia Umoja wa Afrika, AU, Balozi Liberata Mulamula, ameelezea alivyopokea kwa mshtuko kifo cha Mbunge wa Isimani, William Lukuvi kwa malezi bora aliyowapa walipokuwa bungeni.
Akizungumzia msiba huo, leo, Balozi Mulamula alisema kiongozi huyo ndiye alikuwa ‘Chief Whip’ Bungeni alikuwa anawaongoza na kuwaelekeza wabunge.
“Mimi siwezi kusema nilifanya naye kazi maana alikuwa ni kiongozi wetu mwandamizi. Binafsi nilijifunza mengi kisiasa kutoka kwake hususan nikiwa Bungeni alikuwa kama mwalimu kwangu.
“Kwa kweli kifo chake ni pigo kubwa sana Kitaifa. Ameacha pengo kubwa Serikalini na Bungeni,”alisema.
Alisema kiongozi huyo alihudumu miongo kadhaa, ambapo alitoa salaam za pole kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Musa Hassan Zungu, kwa msiba huo mzito kwa nchi yetu.
Aliongeza “Tutamkubuka daima Mhe. Lukuvi kwa utanashati wake, uzoefu wake mkubwa, busara zake na ucheshi. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Mungu awe faraja kwa Mama Lukuvi na watoto katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mpendwa wao. Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe,”.
Taarifa za kifo cha Mbunge Lukuvi, aliyekuwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), ilitolewa jana na Katibu Mkuu Moses Kusiluka, ikieza kuwa umauti ulimkuta kiongozi huyo, jana, Machi 25, alipokuwa akipatiwa matibabu Hospitali ya Benjamini Mkapa,Dodoma kwa tatizo la mshtuko wa Moyo.