Anaswa kwa kujiunganishia huduma ya maji, Mauwasa ikitoa onyo

Maswa. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Maswa (Mauwasa) imeonya wananchi wanaojiunganishia huduma ya maji kinyume cha utaratibu kuacha mara moja tabia hiyo, ikisema itachukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika.

Onyo hilo limetolewa leo Machi 26,2026 na mhandisi wa mamlaka hiyo, Abdulkarim Marik baada ya kumkamata mkazi wa mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa, Haruna Mahamood  akidaiwa kujiunganishia maji kinyume cha utaratibu na kutumia huduma hiyo kwa takribani miezi mitatu bila kulipia huku akiwauzia majirani zake.

Mhandisi wa Mauwasa, Abdulakarim Marik alizungumza mara baada ya kubaini wizi wa maji katika nyumba ya Haruna Mahamood mkazi wa Unyanyembe mjini Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Mhandisi Marik amesema ukaguzi uliofanywa na wataalamu wa mamlaka hiyo ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alisitishiwa huduma kwa kushindwa kulipa deni lake, alikuwa ameunganisha bomba la maji nyuma ya mita hivyo kuendelea kutumia bila kulipia.

“Tumebaini kuwa alifanya muunganisho huo kinyume cha taratibu na kwa muda wa takribani miezi mitatu alikuwa akitumia maji bila kulipia na mbaya zaidi amekuwa akiuza kwa majirani zake. Hili ni kosa kisheria na tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Fundi bomba wa Mauwasa,John Tuma akionyesha jinsi Haruna Mahamood mkazi wa mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa alivyojiunganishia maji kinyume na utaratibu. Picha na Samwel Mwanga

Amesema vitendo vya wizi wa maji vinaathiri mapato ya mamlaka hiyo na pia kusababisha upotevu wa maji ambao unaweza kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengine.

 “Tunatoa rai kwa wananchi wote wanaohitaji huduma ya maji kufika ofisini kwetu ili kupata muunganisho halali. Kujichukulia hatua za kuunganisha maji kinyume cha utaratibu ni kosa na hatua kali zitachukuliwa,” ameongeza.