Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Ireland zimesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuendeleza ushirikiano katika utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupitia programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI.
Kupitia programu hiyo, wanafunzi bora wa kidato cha sita wanapata fursa ya kusoma Shahada ya Kwanza katika masomo ya sayansi ya data, akili unde (AI) na ubunifu katika chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland.
Makubaliano kama hayo yamefanyika pia na chuo kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi, Machi 26, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema makubaliano hayo yanakwenda kufungua fursa zaidi akibainisha huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kupanua fursa za elimu ya juu katika maeneo ya teknolojia na ubunifu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, profesa Carolyne Nombo (kulia ) na makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland nayeshughulikia masuala ya kimataifa, profesa Colin Fitzpatrick (kushoto) wakibadilishana hati ya makubaliano, wanaoshuhudia ni balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Amesema makubaliano waliyoingia yamewezesha kupunguzwa ada kwa asilimia 50 kwa wanafunzi watakaonufaika na programu hiyo, huku mazungumzo zaidi yakiendelea ili kuweza kuongeza nafasi na manufaa kwa wanafunzi wa Kitanzania.
“Tunawapeleka vijana wetu kusoma masomo ya sayansi ya data na akili unde, kule hawaishii darasani tu, bali wanapata fursa ya kufanya kazi na makampuni ya teknolojia huko wanakosoma na kuendeleza ujuzi,” amesema Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda amesema kadri fursa zinavyopatikana ndipo watapanua wigo wa ufadhili kwa wanafunzi, akisisitiza watakaonufaika na mpango huo ni wale tu wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi ili kutoa nafasi sawa kwa vijana kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
“Kwa mwaka huu, wanafunzi 50 wanatarajiwa kunufaika na ufadhili huo, huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kadiri fursa zinavyozidi kupanuliwa,” amesema.
Naye Makamu wa rais wa Chuo Kikuu cha Limerick anayeshughulikia masuala ya kimataifa, Profesa Colin Fitzpatrick, amesema wanafunzi watakaokwenda kusoma nchini Ireland watapata uzoefu wa kimataifa kupitia mafunzo kwa vitendo na fursa za ajira katika kampuni kubwa za nchini humo zinazoshirikiana na chuo hicho.
Naye Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha mapinduzi ya kiuchumi kupitia elimu na ubunifu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, profesa Carolyne Nombo (kulia ) na makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland nayeshughulikia masuala ya kimataifa, profesa Colin Fitzpatrick (kushoto) wakionesha hati ya makubaliano, wanaoshuhudia ni balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Katika kuhakikisha maandalizi bora, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) wanashirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kama kituo cha maandalizi na mafunzo ya awali na ushauri (mentorship) kwa wanafunzi wanaopata ufadhili huo kabla ya kuanza masomo yao nje ya nchi.
Mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI unatarajiwa kuongeza wataalamu wa ndani katika nyanja za teknolojia na ubunifu, huku ukiwapa vijana fursa ya kupata elimu na uzoefu wa kimataifa unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.