Geita. Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amewataka viongozi na makada wa chama hicho kuachana na vinyongo na hasira iliyosababishwa na uchaguzi mkuu uliopita na badala yake waunganishe nguvu katika kuijenga nchi.
Wasira amesisitiza kuwa viongozi wanaoomba kuchaguliwa katika nyadhifa za uongozi ndani ya chama hicho, wana wajibu wa kujifunza na kuielewa misingi ya chama chao, namna uwakilishi kwa wananchi unavyosimamiwa kwa kuzingatia kupigiwa kura kwa hiari ya wanachama.
Wasira ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 26, 2026 wakati wa hotuba yake, Mtaa wa Magogo, Manispaa ya Geita, katika ziara yake ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi za CCM mkoani humo.
Makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi, Ofisi za Chama Mkoa wa Geita.
“Uchaguzi ni gharama na gharama yake nyingine ni hasira tu, ukishindwa unakasirika sana, hiyo nayo ni hasara, unaweza kukasirika lakini ukasirike kidogo tu, maana ukikasirika sana presha ikipanda unaweza ukaugua, halafu ikawa hasara,” amesema.
Wasira amesema uchaguzi haulengi kuwagawa watu bali kuwapata viongozi watakaojitoa kusimamia na kuendeleza mbele malengo endelevu yatakayorahisisha upatikanaji wa huduma za jamii na maendeleo kwa wananchi wanaowaongoza, hivyo kila kiongozi ana wajibu wa kujipima ikiwa anakubalika au hakubaliki kabla ya kuomba kuongoza.
“Unapoomba kuchaguliwa upime watu wanakukubali? Ee, kama hawakukubali unaweza ukakaa ukasubiri mpaka watakapokukubali, lakini kuwalazimisha sidhani kama ni sawa,” amesema.
Jengo la Ofisi za CCM Mkoa wa Geita, ambalo limewekewa jiwe la msingi na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Stephen Wasira, ujenzi umefikia asilimia 94.
Katika hatua nyingine, Wasira ameusifu uongozi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, akimtaja kuwa kiongozi aliyeonyesha uthubutu na msimamo mkali katika kuwatumikia wananchi kwa vitendo akitolea mfano wa kuhamishia makao makuu ya Serikali katika jiji la Dodoma.
“Kuhamisha kwa mwezi mmoja makao makuu kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, huo nao ni uthubutu, kama ungepewa urais wewe wakakwambia huna kazi nyingine isipokuwa kuhamisha watu kwenda Dodoma, ungeweza ukajiuzuru, maana ni kazi ngumu lakini Magufuli alionyesha kuwa uthubutu ni jambo linawezekana,” amesema.
Amesifu namna hayati Magufuli alivyothubutu kupandisha uwekezaji katika sekta ya madini kutoka asilimia tatu hadi asilimia 16, akiutaja kuwa uamuzi mgumu aliouchukua katika kipindi kifupi, akiacha alama ya kudumu ambapo amewataka viongozi ndani ya chama hicho kujifunza kwa kiongozi huyo.
Baadhi ya makada na viongozi wa CCM, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi, Ofisi za Chama hicho Mkoa wa Geita.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila ametoa rai kwa viongozi ndani ya chama hicho kujifunza kutenda na kuyatekeleza yale wanayokuwa wameyaahidi kwa wananchi ikiwa ni moja ya misingi ya uwazi na uwajibikaji wa chama hicho.
Ujenzi wa ofisi za CCM Mkoa wa Geita mpaka kukamilika kwake, unatarajiwa kugharimu Sh1.5 bilioni ambapo hadi sasa fedha zilizotumika katika mradi huo ni Sh1.3 bilioni, fedha hizo zikitokana na wadau mbalimbali waliochangia kupitia harambee iliyofanyika mwaka 2025 na kuongozwa na Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyotolewa na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa ambaye pia ni Katibu wa kamati ya ujenzi huo, Renatus Sangano amesema ujenzi huo umefikia asilimia 94 ambapo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
