Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, Kiwanda cha Tanzania Breweries Limited (TBL) kimeweka mkakati wa kupunguza matumizi ya maji kwenye uzalishaji wa bia na kuhakikisha yote yanayotumika yanachakatwa kabla ya kurejeshwa kwenye mazingira.
Kampuni hiyo imekuja na mpango huo unalenga kulinda rasilimali za maji na viumbe hai, pamoja na kuhakikisha vyanzo vinaendelea kuwa salama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Machi 26, 2026, wakati wa shughuli ya kusafisha mfereji unaotiririsha maji kutoka Mchikichini kuelekea Mto Msimbazi, Meneja wa Kiwanda cha TBL Dar es Salaam, Patel Kilaveli amesema kampuni hiyo inatambua wajibu wake katika uhifadhi wa maji.
“Kama watumiaji wakubwa wa maji, tuna wajibu wa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi rasilimali hii muhimu, kwa kuwa kinywaji tunachotengeneza kinatokana na maji asili,” amesema Kilaveli.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani yanayofanyika Machi 22 ya kila mwaka, yamekuwa fursa ya kutafakari matumizi sahihi ya maji.
“Tumeungana na wadau wengine kutafakari namna bora ya kuhifadhi maji. Kwa kuwa uzalishaji wetu unategemea maji safi, ni muhimu kuyatunza na kuyarejesha salama ili yaendelee kupatikana,” amesema
Kilaveli amesema TBL inalenga kufikia mwaka 2030 kupunguza zaidi kiwango cha maji kinachotumika kuzalisha bia moja, akibainisha kuwa tayari hatua kubwa zimepigwa kuelekea lengo hilo.
Mbali na hatua hizo, kampuni hiyo pia inaunga mkono juhudi za jamii katika kulinda vyanzo vya maji kwa kushirikiana na taasisi nyingine kupitia miradi ya kijamii inayohamasisha uhifadhi wa mazingira.
“Tunawawezesha wakazi wa Ruvu, Kibaha mkoani Pwani kujihusisha na ufugaji nyuki kama njia mbadala ya kipato inayochangia uhifadhi wa mazingira,” amesema.
Kwa upande wa uwekezaji, Kilaveli amesema kiwanda hicho kimewekeza zaidi ya Sh2 bilioni katika mifumo ya kisasa ya kuchakata maji taka.
Wafanyakazi wa kiwanda cha TBL, Dar es Salaam na wakazi wa Mchikichini wkisafisha mfereji wa maji unaotoka Mtaa wa Mission Quarter, Muheza, Mchikichini, unaotiririsha maji hadi Mto Msimbazi, ikiwa ni kuadhimisha siku ya Maji Duniani.
“Tunahakikisha maji yote yanayotoka kiwandani hayaleti madhara kwa mazingira, viumbe hai na binadamu,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wilaya ya Ilala, Adrian Kishe ameipongeza TBL kwa kuboresha miundombinu ya majitaka.
“Kuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma, lakini bado ni muhimu wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira,” amesema Kishe.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam, Teresia Denis amesema uhifadhi wa mazingira ni msingi wa upatikanaji wa maji safi na salama.
“Tunapongeza mchango wa wadau mbalimbali, wakiwemo TBL, katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji,” amesema Denis.
Amesema mfereji wa Mchikichini unaoelekea Mto Msimbazi unakabiliwa na changamoto ya utupaji holela wa taka.
“Mfereji huu unapita katika maeneo ya makazi, hivyo unakumbwa na utupaji wa taka ovyo unaochangia uharibifu wa mazingira,” amesema.
Mkurugenzi wa kampuni ya ukusanyaji taka ya Kajenjele, Mathew Andrew amesema umuhimu wa usafi hasa wakati wa mvua za masika.
Naye Mjumbe wa eneo la Mission Quarter, Muheza B. Mchikichini, Frank Subiri ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu ya mfereji huo.
“Mfereji umejaa mchanga na kusababisha maji kufurika hadi kwenye makazi ya watu, hivyo maboresho ni muhimu ili kudhibiti hali hii,” amesema Subiri.
