Usiri watajwa kichocheo cha mauaji, ukatili

Dar es Salaam. Hivi karibuni, matukio ya ukatili yameendelea kuishtua jamii baada ya watu kadhaa kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

Matukio hayo si ya mbali tena, yanatokea majumbani, mitaani na hata miongoni mwa watu wanaofahamiana, jambo linalozua hofu na taharuki kubwa kwa wananchi.

Miongoni mwa matukio hayo ni kuuawa kwa Athumani Nyanza, ambaye mwili wake ulidaiwa kufukiwa kwenye shimo karibu na nyumba yake, tukio lililozua maswali mengi kuhusu ukatili unaofanyika kwa siri.

Pia, kuna tukio la Linah Kabamba, anayedaiwa kuuawa nyumbani kwake, eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam, kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na mdogo wake, likiwa ni tukio lingine linaloonesha ukatili unaofanyika ndani ya mazingira ya makazi.

Aidha, jijini Mwanza, Rashid Nyandonga anadaiwa kuuawa baada ya kupigwa na mgambo, huku katika Mkoa wa Mbeya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Itumbi, Elia Sambala, akiripotiwa kuuawa katika mazingira yanayochunguzwa.

Matukio hayo, licha ya kutofautiana kwa mazingira na Polisi kuendelea na uchunguzi, yana uzi mmoja unaoyaunganisha, ukatili uliopitiliza na kuporomoka kwa thamani ya maisha ya binadamu na wadau mbalimbali wanasema hali hiyo inaashiria changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa kwa kina, kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Viongozi wa dini wameibuka na tahadhari kuwa kuporomoka kwa maadili na kudhoofika kwa mshikamano wa kiroho ni miongoni mwa sababu kuu zinazochochea ongezeko la vitendo vya ukatili katika jamii.

Wakizungumza na Mwananchi jana Machi 25, 2026, wanasema kadri jamii inavyozidi kuachana na misingi ya imani, ndivyo watu wanavyopoteza dira ya kujitambua, kuvumiliana na kuthamini utu wa mwingine, hali inayofungua mlango wa chuki, hasira na visasi.

Mchungaji wa Kanisa la Kitume, Mbezi, Josephat Mmari, anasema jamii zimekosa mifumo imara ya ushauri na mazungumzo, watu wamechagua kuishi maisha ya kujitenga, wakikosa msaada wa kiroho na kijamii.

Anasema hali hiyo imewafanya wengi kubeba matatizo yao kimyakimya bila kupata nafasi ya kusikilizwa au kuonywa wanapokosea.

“Zamani watu walikaa pamoja, walizungumza, walisaidiana hata kiushauri, leo hii mtu anaumia peke yake, hana wa kumwambia.

“Anajikuta anajaza hasira moyoni hadi inafika hatua ya kulipuka kwa namna ambayo hata yeye mwenyewe hakuitarajia,” anasema Mmari.

Kwa upande wake, Sheikh Abdallah Khamis wa Mbagala jijini Dar es Salaam anasema jamii inahitaji kurejea kwa dhati katika mafundisho ya dini yanayohimiza amani, upendo na hofu ya Mungu.

Anasema imani ya kweli humjenga mtu kuwa na subira na uwezo wa kujizuia hata anapokumbana na changamoto au hasira kali.

“Imani inamfundisha mtu kuvumilia, kusamehe na kufikiri kabla ya kutenda, lakini pale ambapo mtu hana msingi huo, hasira inapokuja inampeleka moja kwa moja kwenye vitendo vibaya bila kujali madhara yake,” anasema Sheikh Khamis.

Anatoa wito kwa jamii kurejesha utamaduni wa kukutana, kusikilizana na kusaidiana, pamoja na kuwahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto katika misingi ya maadili na hofu ya Mungu.

Anasema bila kurekebisha msingi huo wa kiroho, jitihada nyingine zote za kupambana na ukatili zinaweza zisizae matokeo ya kudumu.

Mwanasaikolojia Ramadhani Massenga anasema ongezeko la vitendo vya ukatili vinavyoonekana hivi karibuni si tukio la bahati mbaya, bali ni ubebaji wa matatizo mengi bila kuyashughulikia.

Anasema watu wengi hukosa sehemu salama ya kueleza hisia zao, jambo linalosababisha hisia hizo kujikusanya ndani kwa ndani, na hali hiyo inapofikia kiwango cha juu, mtu anaweza kulipuka kwa hasira na kufanya vitendo vya ghafla.

Anasema mtu anapobeba matatizo mengi bila kuyashughulikia, akili yake inachoka na kupoteza uwezo wa kuchambua mambo kwa utulivu.

“Mtu akipiga ngumi ukutani akiwa na hasira, hiyo ni dalili kuwa angekuwa karibu na mtu angeweza kumpiga, hasira inapofika kileleni, udhibiti unapungua sana,” anasema.

Pia, Massenga anataja matumizi ya mitandao ya kijamii kupita kiasi kuwa ni kichocheo kingine kikubwa cha tatizo hilo, watu kujitenga na mahusiano ya ana kwa ana, hali inayopunguza msaada wa kihisia.

Aidha, anasema wingi wa taarifa unaopokelewa kwa wakati mmoja huzidisha msongamano wa mawazo na kumfanya mtu kushindwa kuchakata mambo kwa usahihi, hivyo kuongeza hatari ya kuvurugika kiakili.

Anasema suluhisho la tatizo hilo ni kurejesha utamaduni wa kuzungumza na kujenga mahusiano ya karibu, watu kushirikisha changamoto zao kwa watu wanaowaamini na kutafuta msaada wa kitaalamu pale inapobidi.

“Ukatili tunaouona leo ni matokeo ya msongo wa mawazo uliopuuzwa kwa muda mrefu. Tukitaka kuudhibiti, lazima tuanze kwa kushughulikia afya ya akili ya jamii,” anasema Massenga.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mpanda, Mkoa wa Katavi, Amina Mponda, anasema kupambana na ukatili kunahitaji mfumo wa kijamii unaojumuisha malezi bora, ushauri wa kihisia na elimu ya jamii.

“Tumekuwa tukikutana na jamii wanapokumbana na changamoto mbalimbali na kuwapatia msaada kisaikolojia, kiroho na kijamii ili kupunguza msongo wa mawazo unaosababisha matukio ya ghafla ya ukatili,” anasema Amina.

Anasema wamekuwa wakitoa elimu kila wanapopata fursa, kwa kushirikisha taasisi mbalimbali na viongozi wa dini zote, ili kusaidia kuondoa sumu zilizopo ndani ya mioyo ya watu, ikiwemo visasi, hasira na tamaa za mali ambazo hawajazitolea jasho.

Kaimu Polisi Jamii, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Christopher Newton, anasema mwezi uliopita, Polisi Kata wameshakaa na jamii katika vikao 1,447, lengo likiwa kutoa elimu kwa jamii juu ya changamoto zinazotokea katika maisha ya kila siku, ikiwemo uhalifu unaoendelea kushuhudiwa nchini.

Anasema vikao hivyo vimehusisha mafunzo na maelekezo juu ya usalama, malezi bora na utunzaji wa maadili katika familia na jamii kwa ujumla.

Newton anasema mojawapo ya changamoto zinazojitokeza ni mmomonyoko wa maadili unaoendelea kuzaa vitendo vya uhalifu na makosa ya jinai.

“Tumeona kuwa pale ambapo jamii inapoachana na misingi ya hofu ya Mungu na maadili mema, ndipo matatizo ya kijamii huanza kuongezeka, jamii huwa na changamoto za kiuchumi, kijinsia na kijamii ambazo zinahitaji uelewa na ushirikiano wa wananchi na Polisi,” anasema Newton.

Vikao hivyo pia vilijikita katika kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa kuangalia malezi ya watoto, kushirikiana na jamii, na kuhakikisha kila mmoja anasimamia nafasi yake.

Anasema malezi sahihi na ufuatiliaji wa kila mwanajamii katika nafasi yake huweza kuzuia uhalifu na kuimarisha hofu ya Mungu miongoni mwa watu.

“Jamii inapaswa kushirikiana kwa karibu, kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri na misingi ya maadili inadumishwa, kwani malezi duni yanasababisha vizazi kuingia kwenye mzunguko wa uhalifu,” anasema.

Aidha, Newton anaweka mkazo kwa viongozi wa dini kutoa elimu endelevu kwa jamii wanayoiongoza, lengo ni kuhakikisha wanajamii wanatambua hatari zinazotokana na vitendo vibaya, kuepukana na migongano ya kijamii na kuunda jamii yenye weledi na hofu ya Mungu.

“Viongozi hawa wanapaswa kuwa mwangaza kwa jamii zao, kuelimisha kuhusu maadili, hofu ya Mungu na umuhimu wa kushirikiana na Polisi Kata ili kudhibiti uhalifu,” anasema.

Matukio mengine ya kusikitisha ni la Naomi Kivamba (13), mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia na kuuawa, jambo lililoibua hasira na majonzi makubwa kwa jamii.

Hukohuko Mbeya, Polisi wanamshikilia Gilbert Mwabulesi (26), mkazi wa Ibililo wilayani Rungwe, kwa tuhuma za mauaji ya baba yake mzazi, Edwin Mwabulesi (65), kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili.

Mkoani Kilimanjaro, Polisi wanamshikilia mkazi wa Kijiji cha Masaera, Reginald Riwa, kwa madai ya kumuua kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili Mwenyekiti wa kitongoji cha Masaera, Ezekiel Temu (62), huku akikimbia na kichwa chake.