WANAWAKE, VIJANA KUNUFAIKA NA MIKOPO NAFUU KUPITIA MFUKO MPYA

Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa VisionFund Tanzania, Deogratias Siria, pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Msaada la Norway (Norwegian Church Aid), Berte Marie Ulveseter, wakisaini makubaliano (MoU) ya kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wanawake na vijana nchini Tanzania yenye thamani ya zaidi ya TZS milioni 200.

      *****

Jamii ya Watanzania, hususan wanawake na vijana, inatarajiwa kunufaika na fursa mpya ya mikopo nafuu itakayosaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kuinua kipato cha kaya.

Mfuko huo wenye thamani ya Sh milioni 200 umeanzishwa na VisionFund Tanzania Microfinance Bank kwa kushirikiana na Norwegian Church Aid (NCA) kwa lengo la kupanua upatikanaji wa mikopo nafuu nchini.

Taasisi hizo zimechangia kwa pamoja rasilimali za kifedha na utaalamu wa kiutendaji ili kuhakikisha mpango huo unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa walengwa.

Kupitia ushirikiano huo, NCA itatoa ufadhili nafuu, kubeba sehemu ya hasara kupitia dhamana ya mikopo pamoja na kufidia riba ili kupunguza gharama kwa wakopaji.

Hatua hiyo itawezesha wananchi kupata mikopo kwa riba ya asilimia 6 hadi 9, kiwango cha chini ikilinganishwa na wastani wa soko wa asilimia 21.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa NCA, Berte Marie Ulveseter, alisema mradi huo unalenga kuwafikia watu wenye mawazo ya biashara lakini wanakosa mitaji nafuu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa VisionFund Tanzania, Deogratias Siria, alisema mpango huo utaenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya fedha na ujasiriamali.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wakopaji kutumia mikopo kwa ufanisi na kuongeza uwezo wa kurejesha.

Kwa ujumla, mpango huu unatarajiwa kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kupunguza vikwazo vya mikopo, na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa VisionFund Tanzania, Deogratias Siria, na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Msaada la Norway (Norwegian Church Aid), Berte Marie Ulveseter, wakipeana mkono baada ya kufanikiwa kusaini Makubaliano (MoU) ya kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wanawake na vijana nchini Tanzania yenye thamani ya zaidi ya TZS milioni 200.