Na Nasra Ismail,Geita.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira, amewatahadharisha wanachama wa chama hicho kuacha tabia ya kuanzisha mivutano na uchochezi wanapokosa fursa za uteuzi au kushindwa katika kura za maoni.
Akizungumza mkoani Geita wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la ofisi za mkoa, Wasira amesisitiza kuwa kukosa uongozi kusitumiwe kama kigezo cha kuvuruga amani ya chama na Taifa, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa nchi.
“Uchaguzi unahitaji ukomavu. Ukishindwa unapaswa kuwa na ‘kifua’ cha kuvumilia matokeo badala ya kuwa chanzo cha mifarakano. Amani ndiyo nguzo kuu ya maisha yetu,” alisema Wasira.
Kiongozi huyo mkongwe alizitaka ofisi za chama nchi nzima kutoishia kuwa majengo tu, bali ziwe vituo vya kutoa elimu ya Katiba na misingi ya CCM ili wanachama waelewe shabaha na malengo ya chama chao.
Aliongeza kuwa kazi ya msingi ya CCM ni kushika dola na kuwaletea wananchi maendeleo, jambo ambalo haliwezi kutimia kama kuna utengano.
Wasira alipongeza juhudi za wanachama na wadau waliochangisha takribani Shilingi bilioni 1.3 kati ya bilioni 1.5 zinazohitajika kukamilisha jengo hilo, ambalo kwa sasa limefikia asilimia 94.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, Nicolous Kasendamila, alibainisha kuwa ujenzi huo ulioanza Mei 2023 unalenga kutoa huduma za kisasa kwa wanachama, huku Katibu Msaidizi wa ujenzi, Renatus Nsangano, akithibitisha kuwa mradi huo ni kielelezo cha namna chama kinavyoweza kujitegemea kupitia nguvu za wanachama wake.





