Iringa/Dodoma. Wananchi wa Jimbo la Isimani, mkoani Iringa wametoa sababu mbalimbali zilizowafanya kumchagua kwa vipindi sita William Lukuvi awe mwakilishi wao bungeni.
Lukuvi (70) amekuwa mbunge wa Islamani (CCM) kuanzia mwaka 1995 hadi jana Jumatano, Machi 25, 2026 alipofariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mshtuko wa moyo.
Mwanasiasa huyo ambaye ndiye alikuwa mbunge mkongwe kuliko wote bungeni, amefariki akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu na mwili wake utazikwa kijijini kwao, Idodi, Ismani Jumanne wiki ijayo.
Leo Alhamisi, Machi 26, 2026, Mwananchi limezungumza na wananchi mbalimbali wa Jimbo la Islamani, kutaka kujua sababu zilizokuwa zikiwafanya tangu mwaka 1995 hadi sasa kumchagua kuwa mwakilishi wao.
Wananchi hao wamesema alikuwa kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi na mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya eneo hilo na alitoa ahadi zilizolenga kuboresha maisha ya wananchi na nyingi zilitekelezwa kwa vitendo.
Sampo Chandindi, mmoja wa wakazi hao amesema tangu alipoanza kugombea ubunge, Lukuvi alitoa nafasi kwa kila kijiji kueleza mahitaji yake, jambo lililosaidia kupanga vipaumbele kulingana na changamoto halisi, hali ambayo ilijenga imani kwa wananchi na kuwafanya waendelee kumchagua.
Wananchi wameeleza uboreshaji huduma za afya kupitia ujenzi wa zahanati katika kata mbalimbali, hatua iliyosogeza huduma karibu yao huku katika sekta ya elimu, ujenzi na ukarabati wa shule umetajwa kuongeza fursa kwa watoto kupata elimu katika mazingira bora.
Agustino Mfikwa, yeye amesema sababu nyingine iliyowafanya waendelee kumpa nafasi ya ubunge, ni kujali kwake wananchi na kushiriki katika shughuli za kijamii, akibainisha alikuwa karibu nao nyakati zote, si kipindi cha uchaguzi pekee.
“Na hali ya upatikanaji wa maji imeboreshwa kwa kiasi kikubwa, tofauti na zamani ambapo eneo hili lilikuwa na changamoto kubwa ya maji,” amesema Mfikwa.
Mkazi mwingine, Jesca Mpalanzi amesema Lukuvi hakuwa kiongozi wa kukaa ofisini pekee, alifika vijijini kusikiliza matatizo ya wananchi na kuchukua hatua na kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ulikuwa miongoni mwa sababu za kuendelea kumchagua.
Pius Kafyome yeye amesema nafasi yake (Lukuvi) serikalini ilirahisisha kufikisha mahitaji ya wananchi na kupata majibu kwa haraka, hali iliyoongeza imani kwa wananchi na pia sifa yake ya uwajibikaji wa kweli katika utekelezaji wa majukumu yake, ni jambo lililosaidia kujenga uaminifu kati yake na wapiga kura.
Kwa upande wake, Brastus Fusi amegusia mchango wa kiongozi huyo katika kukuza sekta ya michezo kijijini hapo, akisema kuwa kupitia juhudi zake, vijana wengi walipata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali, hali iliyosaidia kuwajenga kimwili na hata kuwafungulia fursa nyingine za maisha.
“Alifanya kazi kubwa sana katika sekta ya michezo, vijana walipata motisha na nafasi za kuonyesha vipaji vyao, jambo ambalo halikuwa rahisi kabla yake,” amesema Fusi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Idodi, Christopher Chahe amesema kiongozi huyo alikuwa na nafasi ya kipekee katika jamii, kwani aliweza kujenga uhusiano wa karibu na wananchi na kushiriki nao katika shughuli mbalimbali za kijamii, jambo lililomfanya kupendwa na kuheshimiwa na watu wa rika zote.
Aidha, mwenyekiti huyo amesema katika kipindi chote cha uongozi wake, kiongozi huyo alisimamia na kusaidia utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule mpya na uboreshaji wa zilizokuwepo, hali iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa kijiji hicho.
“Alisaidia sana kujenga na kuboresha shule, watoto wetu walipata mazingira mazuri ya kusoma na kufikia ndoto zao. Hatuwezi kumsahau, aligusa maisha ya wengi wetu na ataendelea kuishi katika kumbukumbu zetu milele,” amesema Chache.
“Sekta ya afya imeboreshwa, huduma zimekuwa karibu zaidi na wananchi na hii imeokoa maisha ya watu wengi,” amesema.
Wakati wananchi hao wakisema hayo, mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema, Patrick Ole Sosopi amesema kitu pekee anachokikumbuka ni muda aliohudumu Lukuvi katika Jimbo la Isimani.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, Lukuvi ndiye mbunge wa kwanza wa Isimani tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi na hakuwahi kupatikana mwingine.
“Tangu jimbo limeanza na siasa za vyama vingi zimeanza, Lukuvi ndiye aliyekuwa mbunge na hadi sasa ndiye aliyekuwa hakuwahi kutokea mwingine,” amesema.
Amesema ni masikitiko kwao kwa kuwa wamempoteza mwananchi mwenzao wa Isimani ambaye kwa umri ni kama baba yake.
“Unajua Lukuvi wakati anaingia bungeni, mimi ndio nilikuwa naanza darasa la kwanza, kwa hiyo kwa umri wake ni kama baba yangu,” amesema Sosopi ambaye amewahi kuingia naye kwenye mbio za ubunge mara kadhaa na kushindwa.
Katika tukio la msiba, amesema yanakosekana mengi ya kueleza kwa kuwa kila kilichotokea ni mpango wa Mungu na sio binadamu.
Kuagwa Dodoma, Dar, Iringa
Ratiba ambayo imetolewa jana Alhamisi ya kuagwa kwa mwili wa Lukuvi utaanza kuagwa leo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Jumamosi ya Machi 28, 2026, mwili wake utaagwa jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Karimjee.
Jumapili ya Machi 29, 2026, mwili wa Lukuvi utasafirishwa kwa ndege hadi Iringa na siku inayofuata Machi 30, utaagwa mjini Iringa eneo la Gangilonga, kabla ya siku hiyohiyo kupelekwa kijijini Idodi, Jimbo la Isimani kwa maziko.
Mazisho ya Lukuvi yatahusisha viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Lukuvi ameacha watoto watatu na mjane mmoja.
Walichopanga na Dk Mwigulu
Jana, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipofika nyumbani kwa Lukuvi, Dodoma kuhani msiba alitaja kitu ambacho kwa mara ya mwisho alipowasiliana na Lukuvi walizungumzia, akisema walikuwa na mvutano kuhusu kikao ambacho kingefanyika juzi.
Dk Mwigulu alisema mvutano huo ulikuwa wa heri kwani yeye (Mwigulu) alitaka kukiahirisha kikao hicho lakini Lukuvi alijenga hoja ya kutaka kisiahirishwe na mwishowe wakakubaliana kiwepo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu hakutaja kikao hicho kilihusu nini na wapi wangekutana. Lukuvi alikuwa ni waziri anayefanya kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Tulipanga kuwa na kikao siku ya jana, mimi nilikuwa napambana kukiahirisha na yeye alipambana kikao kiwepo, kwa hiyo katika mvutano huo, alijenga hoja ikabidi nami nikubali,” amesema Dk Mwigulu.
Aliwataka viongozi wa Serikali na vyama kuendelea kufika nyumbani kwa marehemu Lukuvi na kuwafariji wafiwa akisema katika kipindi hiki, Serikali itakuwa bega kwa bega na familia ili kuhakikisha kila jambo linakwenda vizuri.
