Husain kortini akidaiwa kuiba na kutakatisha cha Sh5 bilioni

Dar es Salaam. Mhasibu Hamid Husain (39) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo ya kughushi stakabadhi za kawaida za malipo,  kutakatisha fedha na kuiba Sh5 bilioni.

‎Mshtakiwa huyo anadaiwa kughushi stakabadhi hizo kwa kuonyesha ni nyaraka halali na zimetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na zimepokea malipo tofautitofauti ya fedha kutoka Kampuni ya Kilimanjaro Cable (T) Limited, wakati akijua kuwa ni uongo.

‎Husain ambaye ni mkazi wa Ocean Road, amefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi Machi 26, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 6592 ya mwaka 2026.

‎Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali Cathbert Mbiling’i, akishirikiana na Ben Lawrence mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

‎Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka yake, hakimu Kiswaga alimueleza mshtakiwa kuwa Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

‎Pia shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo atapelekwa rumande.

‎Hakimu Kiswaga, baada ya kumueleza mshtakiwa huyo upande wa Jamhuri ulimsomewa mashtaka yake.

‎Kati ya mashtaka 43 yanayomkabili 21 ni ya kughushi nyaraka ambazo ni stakabadhi za kawaida za malipo, 19 ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo, mengine ni wizi na kutakatisha fedha.

Mshtakiwa Hamid Husain(39) akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka 43 yakiwemo ya wizi wa Sh5bilioni na kughushi stakabadhi za kawaida za malipo. Picha na Hadija Jumanne

‎Akisomewa mashtaka yake, wakili Mbiling’i alidai katika shtaka la wizi, Husain anadaiwa  kati ya Januari 2020 hadi Februari 2026 eneo la Mikocheni, aliiba Sh5 bilioni.

‎Katika moja ya kughushi nyaraka, wakili Lawrence alidai kuwa Januari 20, 2025 eneo la Mikocheni kwa nia ovu, mshtakiwa alighushi stakabadhi ya kawaida ya malipo ya ushuru, kwa mwaka 2024 hadi Januari 20, 2025 kwa lengo la kuonyesha kuwa nyaraka hiyo ni halali na imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na imepokea malipo ya Sh27 milioni, kutoka Kampuni ya Kilimanjaro Cable (T) Limited, wakati akijua ni uongo.

‎Katika moja ya shtaka la kuwasilisha nyaraka ya kughushi, mshtakiwa anadaiwa katika kipindi hicho na eneo hilo, kwa nia ya udanganyifu aliwasilisha stakabadhi ya kawaida ya malipo kwa Ravish Shah, kwa lengo la kuonyesha kuwa nyaraka hiyo ni halali na imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na imepokea malipo ya Sh27 milioni kutoka kampuni hiyo hiyo ilihali akijua ni uongo.

Upande wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa katika shtaka la kutakatisha fedha, Husain anadaiwa kati ya Januari 2020 hadi Februari 2026 eneo la Mikocheni , mshtakiwa alipokea Sh5 bilioni wakati akujua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la wizi na kughushi nyaraka.

Baada ya kumsomea mashtaka hayo, Jamhuri ilidai kuwa upelelezi haujakamilika hivyo iliomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo uchunguzi umekamilika.

Baada ya kauli hiyo, wakili anayemtetea  mshtakiwa, Josephat Mabula aliomba mahakama itoe maelekezo kwa upande wa mashtaka ili wakamilishe upelelezi kwa wakati.

“Mheshimiwa hakimu, upelelezi kutokukamilika usikwamishe haki zake za msingi mshtakiwa.”

Alidai mteja wake alikamatwa Machi 2, 2026 na amekuwepo Kituo cha Polisi tangu siku hiyo hadi leo siku ya 24 ndio amefikishwa mahakamani.

“Na polisi walimshikilia kwa kipindi chote kwa madai ya kufanya upelelezi na hati ya mashtaka iliyosomwa inathibitisha wazi kuwa upelelezi ulifanyika ndipo mshtakiwa akashtakiwa,” alidai na kuongeza.

“Kama hati ya mashtaka inaonyesha ushahidi wa utendaji kosa, tunaiomba mahakama itoe maelekezo kwa upande wa Jamhuri kuhakikisha kuwa kuahirisha kesi hautakuwa ni sababu ya upelelezi kutokukamilika,” alidai Mabula.

Akijibu hoja, Wakili Mbiling’i alidai kuwa wamemsikia wakili wa utetezi kuhusiana na hoja alizotoa na watazifanyia kazi, lakini upelelezi utakapokamilika watatoa taarifa mahakamani hapo.

“Tutajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi isonge mbele, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia upelelezi umefikia hatua gani,” alidai Mbiling’i

Baada ya maelezo na hoja za pande mbili, Hakimu Kiswaga alielekeza upande wa Jamhuri kamilisheni upelelezi kwa wakati ili mshtakiwa ajue hatima yake na kisha kuahirisha kesi hadi Aprili 9, 2026 itakapotajwa kwa njia ya video.