Bukoba. Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kagera wamekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingilia kati suala la upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa (Nida) kwa maelezo kuwa upatikanaji wake umekuwa changamoto, hali inayosababisha wakose fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kwa vijana.
Maombi hayo yamewasilishwa na wakazi hao pamoja na viongozi wao kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mayunga, mjini Bukoba jana, Alhamisi Machi 26, 2026.
Wamesema wanapohitaji vitambulisho au namba za Nida wanazungushwa, hali ambayo imekuwa kikwazo kwao hata kufikia hatua ya kukata tamaa, hivyo kuziomba Nida na Uhamiaji kutafuta suluhisho la kudumu kwa suala hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Jonston Mutasingwa, amesema amebaini uwepo wa changamoto hiyo baada ya kufanya ziara katika jimbo hilo, ambapo pamoja na mambo mengine alikuwa akihamasisha vijana kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Bukoba.
“Kuna fursa iliyotolewa na Serikali ya Sh200 bilioni kwa vijana, changamoto kubwa ni Nida. Vijana wengi wa Bukoba wanakosa sifa kutokana na kutokuwa na Nida. Naiomba suala hili lifanyiwe kazi kwa haraka ili vijana hawa wanufaike na fursa hii kama ilivyo kwa mikoa mingine,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, amesema suala la vitambulisho hivyo ndani ya mkoa huo limekuwa donda ndugu, hivyo kutoa wito kwa mamlaka husika kuweka mipango na mikakati ili kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi.
Amesema hali ni mbaya zaidi kwa wilaya zilizopo mpakani, ambapo changamoto hiyo inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia wataalamu waliopo na kuomba chama hicho pia kishirikishwe kwenye utatuzi huo.
“Tunajua mkoa wetu unakabiliwa na changamoto ya wahamiaji haramu, lakini hii isiwe kisingizio kwa wale wenye sifa kukosa Nida ili wazitumie hasa kwenye mambo ya kiuchumi. Changamoto hii ya wahamiaji haramu ifanyiwe kazi ili wenye sifa waweze kunufaika na fursa ambazo Serikali inatengeneza kwa ajili ya watu wake, wakiwemo wa Mkoa wa Kagera,” amesema.
Karamagi pia ameiomba Serikali kuhakikisha inatatua changamoto zinazowakabili wananchi katika mkoa huo, zikiwemo za sekta za maji na barabara.
Amesema Mkoa wa Kagera bado haujaunganishwa ipasavyo na mtandao wa barabara, hasa kati ya wilaya za Karagwe na Ngara, Karagwe na Kyerwa, na Bukoba na Kyerwa, hali ambayo kwa namna moja au nyingine inasababisha uchumi wa mkoa na watu wake kushindwa kukua kama inavyotakiwa.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Bukoba wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi.
“Na katika wilaya zote kuna miradi ya maji ambayo imekwama, mfano mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh10 bilioni kule Kyerwa, lakini maji hayatoki. Tunaomba miradi hii ikamilike ili wananchi wapate maji kabla ya mwaka 2030,” amesema.
Mkazi wa Bukoba, Watson James, amesema upatikanaji wa vitambulisho au namba za Nida ni changamoto iliyodumu ndani ya mkoa huo kwa muda mrefu, na kwamba inatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Loyce Rweyunga amesema utaratibu ufanyike ili wale wanaodhaniwa kuwa si Watanzania warudishwe nchini kwao au wafuate taratibu za kuishi nchini, huku akitaka wengine wenye sifa wapewe vitambulisho hivyo kwani ni haki yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Kihongosi amesema Chama cha Mapinduzi kitahakikisha kinaisimamia Serikali ili wananchi wapate maendeleo kama kilivyoahidi.
Amewataka viongozi wa chama na Serikali kusimamia haki na kutotumia nafasi zao kuwanyanyasa wananchi, badala yake wawahudumie kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni ili waweze kunufaika na mipango na mikakati iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya watu wake.
Amewataka Watanzania kuishi kwa upendo, amani na mshikamano, huku akiwataka waepuke wanasiasa wenye nia ya kuwatumia kuleta machafuko nchini, akieleza kuwa kila mmoja ana haki ya kufurahia amani ya nchi.
Amewataka viongozi wa dini pia kutokuruhusu madhabahu katika nyumba za ibada kutumika kutoa hotuba za kuwachonganisha na kuwagawa Watanzania, akisema nyumba za ibada zinapaswa kutumika kuunganisha Watanzania wote.
“Kuna watu wanatumia madhabahu kwenye nyumba zetu za ibada, badala ya kuwaunganisha Watanzania kupitia Mungu wao, wanataka kutugawa. Watanzania tusikubali jambo hili. Kamwe asitokee mtu kwa itikadi ya dini, siasa, ukanda, ukabila wala rangi atugawe,” amesema.
Kihongosi pia amesema kumeibuka tabia ya baadhi ya watu kuhamasisha wananchi kuvichukia vyombo vya dola, jambo ambalo si jema kwa ustawi wa nchi, hivyo kuwaomba wananchi kuheshimu vyombo hivyo kwani vina mchango mkubwa katika ustawi wa taifa na watu wake.
“Hebu chukulia mfano polisi waende likizo na vyombo vingine vya usalama viende likizo nini kitatokea hapa nchini? Je, umewaza kuhusu usalama wa nchi yetu, usalama wako na raia wengine pamoja na mali zao, usalama wa mipaka yetu? Hivi vyombo vina mchango mkubwa kwetu na kwa nchi yetu; tunatakiwa kuvipa ushirikiano na kuwapa moyo,” amesema.
