Balozi Mteule wa Tanzania nchini Oman, Mheshimiwa Maulidah Hassan, amefanya ziara ya kumuaga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Kombo amempongeza Balozi Maulidah kwa kuaminiwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mchango wake alioutoa alipokuwa Msaidizi Binafsi wa Rais katika masuala ya diplomasia.
Aidha, amemsisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Oman, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji na utalii, pamoja na kulinda maslahi ya Watanzania wanaoishi nchini humo, huku akimhimiza kutumia uzoefu wake kuendeleza uhusiano huo.
Kwa upande wake, Balozi Maulidah amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyompa na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu. Amesema pia kuwa amedhamiria kuendeleza diplomasia ya uchumi na kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Oman.
