KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema miongoni mwa makocha bora na wa kisasa anaowatazama zaidi katika Ligi Kuu Bara na kuvutiwa na kazi wanazofanya, ni Mrundi Etienne Ndayiragije wa TRA United na Miguel Gamondi wa Taifa Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ally amesema Ndayiragije ni kocha mzuri wa kisasa aliyemfundisha mambo mengi tangu wakiwa wote Mbao FC ya Mwanza na baadaye kutua KMC, jambo ambalo lilimfanya kuzidi kuonekana kutokana na kazi kubwa aliyofanya.
“Ndayiragije ni kocha ambaye kwangu atabakia mtu muhimu sana, kwa Gamondi sio kwamba tu kwa sababu nimefanya naye kazi timu ya taifa ya Taifa Stars, isipokuwa anajua kufundisha soka la kisasa na kuishi na kila mmoja vizuri,” amesema Ally.
Ally amesema mbali na makocha hao mwingine ni Youssouph Dabo, raia wa Senegal, aliyewahi kufundisha Azam kutokana na ubora wa mbinu zake na kutambua mahitaji ya soka la kisasa.
“Dabo ni kocha anayependa kujifunza mara kwa mara vitu vipya. Kwangu ni mtu ninayependa kumfuatilia kwa sababu anapenda kujua soka la kisasa linahitaji nini na kwa wakati gani. Binafsi makocha niliowataja wanajua wanachofanya.”
Ally alianza kazi ya ukocha katika kituo cha michezo ambacho mmiliki wake ni kocha wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, marehemu, Sylivester Marsh cha jijini Mwanza, aliyesifika kwa upole wake, weledi na misimamo yake awapo kazini.
Baadaye Ally alitua Mbao alipoitwa na aliyekuwa kocha mkuu kwa kipindi hicho, Ndayiragije, alipokabidhiwa kikosi hicho baada ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2016-2017, huku wakiiwezesha kufika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho la FA.
Mbao ilifika fainali hiyo na kukosa ubingwa kwa kuchapwa mabao 2-1 dhidi ya Simba, kisha Ally na Ndayiragije wakatua KMC, kabla ya Mrundi huyo kumuacha mwenzake na kupata dili la kutua Azam.
Baada ya Ndayiragije kutua Azam, Ally akabaki KMC akifanya kazi na Faraji Muya aliyeungana naye katika kikosi cha Tanzania Prisons, akihudumu nafasi ya kocha wa viungo, ingawa wote kwa sasa wapo JKT Tanzania.
