Huu hapa wasifu wa Lukuvi, siku 25,790

Dodoma. Saa 1:00 asubuhi ya Machi 25, 2026, William Vangimembe Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

Lukuvi, akiwa na miaka 70 na Mbunge wa Isimani, Mkoa wa Iringa, aliyeliongoza jimbo hilo kwa miaka 31, amefariki dunia. Mwili wake utazikwa Jumanne kijijini kwao Idodi, Iringa Vijijini.

Leo Ijumaa, Machi 27, 2026, wabunge wanauaga mwili wa Lukuvi katika viwanja vya Bunge. Viongozi mbalimbali wamehudhuria safari hiyo ya mwisho ya mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. Jim Yonazi, amesema wasifu wa Lukuvi. Wasifu huo wote tangu kuzaliwa hadi kifo huu hapa chini:-

Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1955 katika kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoa wa Iringa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri aliyeshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na alijulikana kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi, uzalendo, pamoja na uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi. Aliweka maslahi ya Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Alijulikana kwa mtindo wake wa kazi wa kutembelea maeneo ya miradi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali. Katika kudhihirisha uchapakazi wake, siku moja kabla ya umauti kumkuta, marehemu alihudhuria na kuratibu shughuli za Serikali katika vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970.

Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) kuanzia mwaka 1974 hadi 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa Cheti cha Ualimu.

Mwaka 1982–1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa (Advanced Diploma in Political Science).

Alipata Shahada ya Masuala ya Kimataifa na Diplomasia (Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy) kutoka Washington International University kuanzia mwaka 1999 hadi 2001. Baadaye alijiendeleza katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa mwaka 2008–2011.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga na Chama cha TANU akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika chuo hicho mwaka 1974–1975.

Mnamo mwaka 1984 alichaguliwa kuwa mjumbe wa vikao vya Umoja wa Vijana wa CCM katika ngazi ya wilaya hadi taifa. Alichaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa na Wilaya wa Chama cha CCM mwaka 1980–1984. Vilevile, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka 1993–1994. Aidha, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Chama mwaka 2010 hadi sasa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi aliajiriwa kama mwalimu katika Wizara ya Elimu kuanzia mwaka 1975 hadi 1980. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuanzia mwaka 1994–1995, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma 2006–2008 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam 2008–2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa nchini uliofanyika mwaka 1995, Marehemu Lukuvi alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na hivyo kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo, alilolitumikia kwa takribani miaka 30 hadi umauti ulipomkuta. Akiwa mbunge aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuanzia mwaka 2005–2010.

Katika maisha yake ya siasa, Marehemu Lukuvi aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira mwaka 1995–2000. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu na Mnadhimu Mkuu wa Serikali (Chief Whip) kati ya mwaka 2000–2005, 2010–2015 na 2025–2026.

Halikadhalika, Marehemu Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia Januari 2015 hadi mwaka 2022. Aidha, mnamo Juni 2023, aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais kuhusu Mahusiano ya Kisiasa na Kijamii.

MAFANIKIO KATIKA SEKTA ALIZOONGOZA

Akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu):

  • Alikuwa msimamizi mahiri wa shughuli za Serikali Bungeni na aliimarisha mahusiano kati ya Serikali na Bunge.
  • Alisimamia utekelezaji wa sera za kuboresha ustawi wa watu wenye ulemavu.
  • Alisimamia kikamilifu ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
  • Alisimamia maboresho ya mifumo ya usimamizi wa maafa nchini.
  • Alihakikisha wizara zote zinafanya kazi kwa ushirikiano katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi:

  • Alitatua migogoro ya ardhi kwa kuanzisha mifumo bora.
  • Alianzisha mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa ardhi.
  • Alisimamia utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya 1,992,245.
  • Alitenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kuongeza ajira.

Akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM:

  • Alianzisha mfumo wa mbio za mwenge kwa ushindani wa mikoa.
  • Alianzisha mradi wa mabasi ya wanafunzi Dar es Salaam.

Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma:

  • Alifufua kilimo cha mtama na kuanzisha mashamba ya zabibu.
  • Aliimarisha mipango ya miji kuzuia ujenzi holela.
  • Alisimamia ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDOM.

Enzi za uhai wake, Marehemu Lukuvi alifunga ndoa tarehe 28 Julai 1990 na Bi. Germina Lukuvi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Dar es Salaam, na kujaaliwa watoto watatu: Nobert William Lukuvi, Brown William Lukuvi na Anifisye Vanessa William Lukuvi.

Ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwaye Donovan.

Marehemu William V. Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi 2026 saa 1:00 asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata mshtuko wa moyo.

Tangu kuzaliwa hadi kifo, ameishi duniani siku 25,790.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya William V. Lukuvi ambaye aliitumikia nafasi yake ya ubunge na nyadhifa nyingine kwa bidii, ufanisi na uadilifu wa hali ya juu. Tunaomba Mungu ampe pumziko la amani.

RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA, NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE. APUMZIKE KWA AMANI, AMINA.