Ng’ondya: Geita Gold haikamatiki, atuma salamu kwa wapinzani

KIUNGO mshambuliaji wa Geita Gold, Richardson Ng’ondya, amesema licha ya tofauti ndogo ya pointi na wapinzani wao msimu huu, wasitarajie kuwa rahisi kuikabili timu yake kutokana na mikakati imara waliyojiwekea ya kufanikisha malengo yao.

Ng’ondya amesema ubora wa benchi la ufundi na wachezaji wa kikosi hicho unawapa motisha ya kuipambania timu hiyo ili irejee tena Ligi Kuu, baada ya kushuka msimu wa 2023-2024, licha ya ushindani mkali kutoka kwa wapinzani.

“Licha ya Ligi kusimama, tunaendelea na mazoezi kuhakikisha hatutoki nje ya malengo tuliyojiwekea. Tunatambua wazi kuwa mechi hizi za mwishoni ni ngumu kutokana na kila timu kutaka matokeo, lakini tutapambana hadi mwisho,” amesema Ng’ondya.

Nyota huyo, aliyecheza Azam FC chini ya miaka 20, African Sports, Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mbeya City, alijiunga na Geita Gold msimu huu baada ya kuachana na Kagera Sugar, huku tayari ameshaifungia timu yake mabao manne.

Geita, iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, iliimaliza nafasi ya nne na pointi 56 msimu wa 2024-2025 wa Championship chini ya Kocha Mkuu Mohamed Muya, baada ya kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara.

Kikosi hicho kilicheza mechi za Play-Off dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’, iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61, na kuondolewa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kupoteza ugenini 2-0.

Msimu huu, Geita imeonyesha kiwango bora, ikipoteza mechi moja tu kati ya 21. Kichapo hicho kilikuwa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania, mechi iliyopigwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, Februari 20, 2026.

Hadi sasa katika msimu wa 2025-2026, Geita imeshinda mechi 16, sare nne na kupoteza mmoja tu kati ya 21, ikiongoza kileleni kwa pointi 52, ikifuatiwa na Kagera Sugar ya pili ikiwa na pointi 49, baada ya kushinda mechi 15, sare nne na kupoteza mechi mbili.