Serikali kujenga soko la kisasa, daraja Muleba

Muleba. Wakulima na wafanyabiashara wilayani Muleba mkoani Kagera wanatarajia kunufaika na ongezeko la fursa za biashara na usafirishaji wa mazao baada ya Serikali kutekeleza miradi ya zaidi ya Sh14.4 bilioni ya ujenzi wa soko la kisasa na daraja jipya la Kamshago.

Miradi hiyo ambayo ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji inatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa wilaya hiyo pamoja na maeneo ya jirani ndani ya Mkoa wa Kagera.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa soko kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, leo Machi 27, 2026, Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Wilaya ya Muleba, Mary Joseph, amesema ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 91 ya utekelezaji.

Amesema soko hilo la kisasa linatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh1.9 bilioni, ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa zaidi ya Sh1.6 bilioni.

“Jengo hili la ghorofa moja litakapokamilika litakuwa na jumla ya vyumba 84 kwa ajili ya wafanyabiashara. Mradi upo katika hatua za mwisho ili uweze kukabidhiwa kwa mteja na kuanza kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mary.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa soko unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh1.9 bilioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Mbali na soko hilo, Serikali pia imekamilisha ujenzi wa Daraja la Kamshago ambalo limegharimu zaidi ya Sh12.5 bilioni, likilenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji katika eneo hilo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Samuel Mwambungu amesema daraja jipya limejengwa kuchukua nafasi ya daraja la zamani lililokuwa dogo na chakavu.

Amesema daraja hilo la awali lilikuwa changamoto kwa watumiaji wa barabara kwa sababu magari yalilazimika kupokezana kutokana na upana mdogo.

“Mradi huu umekamilika na sasa mkandarasi anamalizia kazi ndogo ndogo ikiwemo usimikaji wa taa kabla ya kukabidhi rasmi. Hata hivyo daraja tayari limeanza kutumika na kwa sasa magari yanaweza kupishana tofauti na daraja la zamani,” amesema Mwambungu.

Baadhi ya wakazi wa Muleba wanasema kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta nafuu kubwa kwa wananchi, hasa wakulima waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.

Emiliana Saasita, mkazi wa Muleba, amesema daraja la Kamshago limekuwa mkombozi kwa wakulima waliokuwa wakipata wakati mgumu kusafirisha mazao yao.

“Awali tulikuwa tunapata shida kubwa kupitisha mazao kutoka mashambani kuja sokoni kwa sababu ya daraja dogo. Sasa hali hiyo haitakuwepo tena na mazao yatafika sokoni kwa urahisi,” amesema.

Kwa upande wake, Victor Mwengi amesema ujenzi wa soko la kisasa utachochea ukuaji wa biashara kwa kuwa wafanyabiashara wengi watapata sehemu rasmi ya kufanyia shughuli zao.

Akizungumza baada ya kukagua mradi wa soko hilo, Kihongosi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kwa kutumia mapato ya ndani kugharamia ujenzi wa soko hilo.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa dhana ya kujitegemea na kuongeza kuwa soko hilo litakuwa chanzo muhimu cha mapato kwa halmashauri pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi.

“Hili si jambo dogo. Mmeweza kutumia mapato yenu ya ndani kujenga soko hili ambalo mbali na kuwa kitega uchumi kwa halmashauri pia ni sehemu ya kuboresha huduma kwa jamii. Hongereni sana kwa kutekeleza ajenda ya kujitegemea kwa vitendo,” amesema.

Kihongosi amezitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano huo kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani ili kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa soko unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh1.9 bilioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Kuhusu daraja la Kamshago, amesema kukamilika kwake ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa za kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi.

Amesema miradi hiyo inaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali.

“Chama hiki kikiahidi kinatekeleza. CCM ikiahidi inatenda, na hutenda kadri rasilimali zinavyopatikana kwa sababu maslahi ya wananchi ndiyo kipaumbele chetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuisimamia Serikali kuhakikisha miradi yenye tija kwa wananchi inaendelea kutekelezwa kadri fedha zinavyopatikana.