Mapya raia aliyeshambuliwa Afrika Kusini

Dar es Salaam. Baada ya video kusambaa kwenye mitandoa ya kijamii ikimuonyesha kijana aliyedaiwa ni Mtanznaia akishambuliwa nchini Afrika kusini, Balozi wa Tanzania nchini humo, James Bwana amesema huyo sio Mtanzania.

Tukio hilo linalokanushwa na Balozi Bwana ni video ilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha kijana akishambuliwa huku kukiandikwa maneno ya kuonyesha kijana huyo ni raia wa Tanzania, madai hayo yamekanushwa na balozi.

Kupitia video hiyo fupi iliyotumwa mtandaoni kijana huyo wa kiume akiwa kwenye duka lake, alitakiwa kuonyesha nyaraka za uwepo wake nchini humo ambazo alizionyesha akitamka neno ‘valid’ikiwa na mana ziko sawa.’

Hata hivyo, alianza kutandikwa viboko sehemu za juu ya mwili wake akitakiwa kufunga duka lake.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo leo Ijumaa, Machi 27, 2026 Balozi Bwana amesema wamedhibitisha kijana huyo sio raia wa Tanzania.

“Baada ya kufuatilia tumebaini huyo sio raia wa Tanzania,” amesema Balozi Bwana.

Awali, Balozi Bwana alipozungumza na Mwananchi juu ya tukio hilo alisema wameliona na wanalifuatilia kubaini undani wake na kama kweli raia huyo ni wa Tanzania.

“Tumeiona video japo ni ngumu kufahamu kama huyo ni Mtanzania kwa kuangalia, kwahiyo tunafuatilia kujua kama ni kweli huyo ni Mtanzania mwenzetu na sio video ya kutengeneza Ai,

“Kama kuna mtu anamfahamu anaweza kutusaidia kwa haraka ni wapi alipo na mawasiliano yake,”amesema.

Balozi Bwana amesema zipo oparesheni zinaendelea huko Afrika kusini kudhibiti wahamiaji haramu akiwataka Watanzania wanaokwenda nchi za watu kuhakikisha wanafuata utaratibu.

Amesema wapo baadhi ya watu hukimbilia mataifa hayo kupitia njia za panya na kuishi wanavyoishi, yanapotokea matatizo huwakumba kutokana na utaratibu mbovu waliotumia kuingia nchi hizo.

Balozi Bwana amesema wapo raia kutoka mataifa mbalimbali wanaopitia changamoto Afrika kusini na mataifa mengine kutokana na matatizo yao ya kutofuata utaratibu wa uhamiaji.

“Kama ataondoshwa nchini ni moja hakuwa na vibali vya kuishi huko na hana vibali halali vya kuonyesha kuwa yupo kihalali inakuwa ni ngumu kuingilia maana inakuwa ni utaratinu wa uhamiaji na huo upo mataifa mengi tu,”amesema.