Simanjiro. Onyo kali limetolewa kwa baadhi ya viongozi wa vijiji wilayani Simanjiro mkoani Manyara wanaodaiwa kujihusisha na uuzaji holela wa ardhi, huku Mkuu wa Wilaya hiyo akisisitiza kuwa tabia hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi inayoongezeka katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amewataka viongozi hao kusitisha kuuza ardhi ya kijiji kinyume cha sheria, akionya kuwa yeyote atakayebainika kuendeleza mtindo huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Lulandala ametoa kauli hiyo Machi 27, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nadonjukin, Kata yaKomolo, uliolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amesema baadhi ya viongozi wa vijiji wamegeuza uuzaji wa ardhi ya kijiji kuwa chanzo cha kipato binafsi, hali inayochochea migogoro ya ardhi na kuathiri amani ya wananchi.
“Ardhi ni urithi wa jamii kwa vizazi vyote. Ni wajibu wa viongozi kuhakikisha inatunzwa na kugawiwa kwa kufuata sheria na taratibu ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima,” amesema Lulandala.
Ameonya kuwa ardhi ni rasilimali isiyoongezeka hivyo inahitaji usimamizi makini ili kulinda maslahi ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
“Tusipofuata sheria tunawaumiza wananchi wetu wenyewe. Ardhi ikisimamiwa vibaya inaleta migogoro, chuki na wakati mwingine hata vurugu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota amesema Serikali imeweka taratibu za wazi za ugawaji wa ardhi ambazo zinapaswa kufuatwa na kila kijiji.
Makota amesema ugawaji wa ardhi unaruhusiwa tu katika vijiji vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi uliopitishwa na Baraza la Madiwani.
“Hatua hii inalenga kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali hii muhimu na kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza katika jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa maombi yote ya ardhi yanapaswa kuwasilishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya uchakataji, huku akisisitiza kuwa vijiji vyenye migogoro ya ardhi havitaruhusiwa kugawa maeneo mapya hadi pale migogoro hiyo itakapopatiwa ufumbuzi.
Hatua hiyo ya viongozi wa wilaya inalenga kurejesha utaratibu katika usimamizi wa ardhi, kupunguza migogoro ya mara kwa mara na kulinda maslahi ya wananchi kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nadonjukin wamesema baadhi ya viongozi wa vijiji wamekuwa chanzo kikuu cha uuzaji holela wa ardhi na kusababisha migogoro isiyoisha.
Mkazi wa kijiji hicho, Joshua Mollel, amesema baadhi ya wenyeviti wa vijiji wamekuwa wakigawa ardhi kiholela kwa maslahi binafsi.
“Hao baadhi ya wenyeviti wa vijiji ni walanguzi wa ardhi. Wanagawa maeneo kama chakula cha njaa na kusababisha migogoro isiyoisha katika vijiji vyetu,” amesema Mollel.
Naye Naishiye Jackson, mkazi mwingine wa eneo hilo, amesema baadhi ya viongozi hushirikiana na watu wachache kuuza ardhi kwa kutumia mihutasari isiyo halali ili kujipatia kipato.
Amesema hatua kali zikichukuliwa dhidi ya viongozi wachache wanaobainika kufanya vitendo hivyo, itakuwa funzo kwa wengine na kusaidia kukomesha uuzaji holela wa ardhi katika wilaya hiyo.
“Hili suala linahitaji kukomeshwa. Wakichukuliwa hatua viongozi wachache, wengine wataogopa na kuacha tabia hiyo,” amesema Jackson.
