Matumizi akili unde yanavyolazimisha mageuzi makubwa vyuoni

Dar es Salaam. Matumizi yanayoongezeka ya teknolojia ya akili unde (AI) katika vyuo vikuu yameanza kuibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa mfumo wa mitihani na tathmini za wanafunzi, huku wataalamu wakionya kuwa mbinu za jadi za kupima maarifa hazitoshi tena katika zama za teknolojia hiyo.

Tahadhari hiyo imebainishwa kupitia utafiti uliofanywa na wahadhiri wa Chuo cha Ushirika Moshi, Profesa George Matto na Fransisca Kalatunga, uliopewa kichwa “Mabadiliko ya Mtazamo: Kutafakari upya tathmini za ufundishaji katika elimu ya juu katika enzi za matumizi ya akili unde”

Utafiti huo unaangazia jinsi matumizi ya AI yanavyobadilisha kwa kasi mazingira ya ujifunzaji katika elimu ya juu na kuleta changamoto mpya katika mfumo wa tathmini.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo katika kongamano la kimataifa la uboreshaji elimu na maendeleo endelevu lililofanyika Machi 26, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Matto alisema maendeleo ya AI yamefanya iwe rahisi kwa wanafunzi kupata majibu ya maswali, kuandika maandishi na kufanya uchambuzi wa taarifa kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

Alieleza kuwa hali hiyo imefanya mbinu za tathmini zilizokuwa zikitumika kwa muda mrefu kuonekana kupitwa na wakati.

Mhadhiri wa Chuo cha Ushirika Moshi, Profesa George Matto akiwasilisha matokeo ya utafiti wakati wa kongamano la kimataifa la uboreshaji elimu na maendeleo endelevu lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema mbinu nyingi zinazotegemea kukariri maudhui au kupima matokeo ya mwisho, haziwezi tena kutoa picha sahihi ya uwezo halisi wa mwanafunzi.

“Katika kipindi hiki, mfumo wa tathmini unapaswa kuangalia zaidi mchakato wa kujifunza, uwezo wa kufikiri kwa kina na namna mwanafunzi anavyotumia maarifa kutatua matatizo, badala ya kuangalia majibu ya mwisho pekee,” amesema.

Utafiti huo pia umebainisha changamoto kubwa ya uadilifu wa kitaaluma.

Teknolojia ya AI inaweza kurahisisha udanganyifu kwani wanafunzi wanaweza kuitumia kuandika majibu ya kazi au mitihani bila kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza. Hali hii inaweza kudhoofisha uaminifu wa mfumo wa tathmini unaotumiwa kupima uwezo wa wanafunzi, amesema.

Watafiti wanaonya bila kubadilisha mbinu za tathmini, vyuo vikuu vitaendelea kupima matokeo yasiyoakisi uwezo halisi wa wanafunzi.

Pia, matumizi ya AI yanaweza kupunguza uwezo wa wanafunzi kufanya tafakuri za kina, kwani wanaweza kukwepa hatua muhimu za kujifunza kama kuchambua ushahidi, kuhoji dhana na kutafakari uelewa wao.

Kwa mujibu wa utafiti, kukwepa hatua hizi kunaweza kudhoofisha uwezo wa wanafunzi kujenga hoja, kufanya uchambuzi wa kina na kuendeleza ubunifu.

Aidha, utegemezi mkubwa wa AI unaweza kuathiri uzalishaji wa maarifa mapya, kwani wanafunzi wanaweza kupoteza nafasi ya kujifunza kupitia uchunguzi na mijadala ya kitaaluma.

Profesa Matto alieleza hali hiyo inaweza kudhoofisha jukumu la vyuo vikuu kama vituo vya uzalishaji wa maarifa.

Mhadhiri wa Chuo cha Ushirika Moshi, Profesa George Matto akizungumza na mwandishi wa Mwananchi (hayuko pichani) wakati wa mahojiano.

Utafiti pia umebaini changamoto ya usawa katika tathmini, ambapo wanafunzi wenye ufikiaji mkubwa wa teknolojia au ujuzi wa kuitumia, wanaweza kupata faida zaidi kuliko wenzao, jambo linaloweza kuongeza pengo la kielimu.

Matokeo haya yameibua mjadala miongoni mwa wadau wa elimu kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sebastian Kilindima, amesema badala ya kupiga marufuku AI, ni muhimu kubadilisha mfumo wa tathmini ya ujifunzaji ili kupima ujuzi wa juu zaidi.

“Teknolojia ya AI haiwezi kuzuiwa. Kilicho muhimu ni kuboresha mfumo wa tathmini ili kupima uwezo wa kufikiri, kuchambua na kutatua matatizo,” alisema.

Mdhibiti ubora wa elimu, Mathias Kitwanga, alisema AI inaweza kuwa na manufaa makubwa endapo itatumika kwa mwongozo sahihi. Amesisitiza walimu wanapaswa kuwafundisha wanafunzi kuitumia kama nyenzo ya kujifunzia, si njia ya kukwepa kazi.

Matilda Lyimo ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Dar es Salaam amesema zana za akili mnemba zimekuwa msaada mkubwa katika kutafuta taarifa na kupanga mawazo ya kazi za kitaaluma.

Hata hivyo, amesisitiza wanafunzi wanapaswa kuwa waangalifu ili wasitegemee teknolojia hiyo kupita kiasi.

“Akili mnemba inaweza kusaidia kupata mwongozo wa awali wa mawazo, lakini bado tunapaswa kusoma na kuelewa masomo yetu kwa kina,” amesema.

Kutokana na changamoto hizo, utafiti huo unapendekeza mageuzi katika mfumo wa tathmini vyuoni.

Profesa Matto amesema miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuimarisha tathmini za ushirikiano zinazohusisha wanafunzi kufanya kazi kwa pamoja katika kutatua changamoto za kitaaluma.

Pia inapendekezwa kuongezwa kwa tathmini zinazopima uwezo wa kufikiri kwa kiwango cha juu kama vile uchambuzi, ubunifu na utatuzi wa matatizo.

Aidha, utafiti huo umeshauri matumizi makubwa ya tathmini halisi zinazoweka wanafunzi katika mazingira yanayofanana na changamoto halisi wanazoweza kukutana nazo katika jamii au katika kazi zao baada ya kuhitimu.

Mbinu nyingine inayopendekezwa ni tathmini za miradi ambazo zinahitaji wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kubuni, kuchunguza na kutekeleza mawazo yao.

Kwa mujibu wa Profesa Matto, mageuzi hayo ni muhimu ili kuhakikisha mfumo wa elimu unaendelea kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kufanya kazi kwa ushirikiano na kutatua changamoto za dunia ya sasa inayozidi kutegemea teknolojia.