Mbeya. Wakati vilio, simanzi na majonzi vikiendelea kutawala katika familia zilizopoteza wapendwa wao katika maporomoko yaliyoua watu 20 na kujeruhi kadhaa wilayani Rungwe, majeruhi wamfunguka undani wa tukio wakiiomba serikali kuwasaidia.
Machi 25, wananchi wa Kata za Lupepo, Nkunga, Kawetele na Ikuti wilayani humo, mkoani Mbeya, walikumbwa na taharuki ya maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku na kusababisha hasara za mali, vifo na majeruhi.
Baadhi ya familia zilipoteza ndugu, jamaa na marafiki, ikiwamo waliopoteza watu wanne wa familia moja, wengine wakipoteza watatu, wawili na wengine mmoja mmoja, huku kuzuka taharuki, simanzi na vilio.
Wakizungumza na Mwananchi iliyofika katika maeneo hayo, baadhi ya majeruhi walionusurika katika tukio hilo wameeleza jinsi walivyopoteza wapendwa wao na namna wenyewe walivyonusurika kifo kutokana na mvua hiyo.
Aneth Mwaluhande amesema majira ya saa 5 usiku mvua kubwa ilinyesha, ambapo nyumba waliyokuwamo wakajikuta wanaangukiwa na ukuta akiwa na mama yake na mtoto wake, ambapo aliona dalili za kifo.
Amesema wakati wa harakati za kujipambania uhai, aliangukia kwenye shimo la maji akiambaa ambaa na maji ambayo yalikuwa yanaongezeka, akawa anasukuma maji hayo na udongo.
“Nilipofanikiwa kutoka nyumba, ikawa haionekani, nikahisi mama na mtoto wangu wamekufa. Ile nafika chini kwa kaka yangu, nakutana na mtoto wangu anasema haelewi alifikaje huko chini.”
“Nikawa sijielewi. Kaka akaita watu wakatoa msaada, tukafikishwa hospitali na daktari akatupa huduma. Watu wakaendelea kumtafuta mama yangu aliyekuwa amemezwa na tope na kujikuta amekufa,” amesema Aneth.
Akielezea namna alivyopigania uhai wa mama yake licha ya juhudi zisizotoa matunda, Michael Mwaluhande amesema baada ya kuitwa na mdogo wake (Aneth) alifika nyumbani na kukuta udongo umemfukia mama yake.
“Nilifika mama alipokuwa amezama. Nilikuwa sijavaa nguo, nikaona nitakufa mimi wakati udongo ukiendelea kushuka. Serikali ilifika, tukapambana, ila haikuwa bahati yetu; yote tunamshukuru Mungu.
Hakuna tulichoookoa ndani, nyumba imebomoka, mbolea aliyokuwa anauza mama ikaharibika, pesa aliyokuwa nayo ikapotea. Serikali itusaidie; hatuna jinsi ya kuishi hapa, hatuna pakwenda,” amesema Michael.
Mtoto Noel Mwakijungu amesema akiwa amelala alisikia mawe yakianza kumdondokea huku maji yakimsukuma nje, na alipoamka akachukua kitenge kujifunika kabla ya mama yake kumsaidia.
“Ilikuwa usiku nimelala ghafla nikasikia mawe yananidondokea, baadaye maji yakawa yananisukuma nje kwenye mkahawa. Nikashika kitenge kujifunika, ndio mama akafika kunisaidia,” amesema Mwakijungu.
Banord Kasambala, aliyepoteza watoto wawili na mke wake, amesema mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 25 iliacha simanzi kwake kwa kuwapoteza wapendwa wake, ambapo alinusurika tu.
“Mimi udongo haukunifunika kichwani kama ilivyokuwa kwa watoto na mke wangu. Ndugu zangu walifika kutusaidia kwa kuiokoa familia yangu, lakini wenzangu walifariki. Nimebaki peke yangu,” amesema Kasambala.
Naye Victor Mbuya, mkazi wa Kitongoji cha Mabwe, amesema madhara yaliyowakuta ni makubwa na ni tukio la kwanza katika maisha yao, akieleza kuwa amewapoteza wazazi na watoto wake.
Ameiomba serikali kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu na kuona namna ya kuboresha miundombinu, haswa barabara, ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.
“Tunaomba serikali itusaidie. Kwa sasa barabara zimeharibika, hata ikihitajika mtu kusafiri hali si nzuri sana. Madhara yaliyotukuta ni makubwa mno, tunaomba msaada wao kwa sasa,” amesema Mbuya.
Akisimulia ilivyokuwa, Victoria Moto amesema akiwa amelala ndani na watoto, walisikia mvua kubwa akiamini ni tetemeko la ardhi, ambapo alishuhudia maji mengi yakiingia ndani na kuwawahi watoto waliokuwa wanashindwa kutoka chumbani.
“Nashukuru Mungu wote ndani tulipona, japokuwa madhara ni makubwa. Chakula tulichokuwa nacho ndani kiliharibika, nguo zote zimesombwa na tope, nyumba imeharibika. Tunaomba msaada,” amesema Victoria.
Kwa upande wa Emanuel Kananika, mkazi wa kijiji cha Lupepo, amesema mvua ilianza kunyesha saa 3 usiku, ambapo akiwa na mwenzake Athuman katika mazungumzo ya kawaida, wakajikuta wamezingirwa na maji.
“Nilianza kumuita mwenyekiti wa kitongoji changu, Lucas Mwafyela, tukiomba msaada, lakini baadhi ya familia tulipoteza ndugu watatu na jirani yangu akapoteza wanne. Kwa ujumla tunayo masikitiko,” amesema Kananika.
Akizungumzia athari ya mafuriko hayo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mabwe, Inocent Fredmoto, amesema katika eneo lake watoto watatu wamefariki dunia, huku nyumba zaidi ya saba zikibomoka na mashamba yakiharibika.
“Miundombinu ni tatizo; kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine haiwezekani. Serikali itusaidie kwa chochote. Mazao yameharibika, chakula hakuna kwa sasa, jamii inatahabika,” amesema Mwenyekiti huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu amewataka wananchi kuhama maeneo hatarishi kwa kipindi hiki mvua zikiendelea kunyesha ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesema wakati wananchi hao wakiondoka maeneo hatarishi, serikali inaendelea kuangalia cha kufanya kwa siku za mbeleni, akieleza kuwa mvua kwa sasa ni nyingi katika Wilaya hiyo.
“Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, naomba wananchi tuchukue tahadhari. Hatutaki kuona madhara au athari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha; mvua ni nyingi kwa sasa,” amesema Haniu.
