Mwanamke Avunja Rekodi, Aapishwa Kuwa Askofu Mkuu Uingereza

Canterbury, England — Sarah Mullally ameweka historia baada ya kuapishwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury, hatua inayomfanya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Church of England katika historia ya kanisa hilo lenye mizizi ya karne nyingi.

Sherehe hiyo iliyofanyika katika Canterbury Cathedral ilihudhuriwa na wageni takribani 2,000, wakiwemo viongozi wa kifalme kama Prince na Princess wa Wales, pamoja na viongozi wa dini na waumini kutoka maeneo mbalimbali.

Hafla hiyo ilijulikana kihistoria kama “enthronement,” ikiashiria mwanzo rasmi wa huduma yake kama kiongozi wa kiroho.

Katika mahubiri yake ya kwanza, Mullally alieleza kwa hisia kubwa namna maisha yake yalivyobadilika, akisema kuwa yeye akiwa kijana hangeweza kufikiria hatma aliyofikia leo. Alisisitiza umuhimu wa imani, unyenyekevu na utumishi katika uongozi wa kiroho.

Mullally, ambaye alisilimu Ukristo akiwa na umri wa miaka 16 na baadaye kufanya kazi kwa muda mrefu kama muuguzi kabla ya kuingia katika huduma ya kanisa, alisema uzoefu wake katika sekta ya afya na uongozi umemwandaa kwa jukumu hilo kubwa.

Uteuzi wake unakuja wakati Kanisa la England likikabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo tofauti za kiitikadi ndani ya jumuiya ya Anglikana duniani, hususan kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi wa kanisa. Ingawa wanawake waliruhusiwa kuwa mapadri mwaka 1994 na maaskofu mwaka 2015, hatua ya sasa inaonekana kama ukomo wa mabadiliko ya kihistoria ndani ya kanisa hilo.

Katika hotuba yake, Mullally pia aligusia changamoto za kijamii na kiroho duniani, akisisitiza umuhimu wa amani, mshikamano na kushughulikia maumivu ndani ya jamii, ikiwemo yale yanayotokana na migogoro na changamoto ndani ya taasisi za kidini.

Aidha, ameahidi kujikita katika kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha kanisa linakuwa salama kwa waumini wote, hasa katika masuala ya ulinzi wa watoto na watu walio katika mazingira hatarishi, eneo ambalo litakuwa chini ya uangalizi mkubwa wakati wa uongozi wake.

Uteuzi wa Mullally unaonekana kama mwanzo wa enzi mpya katika historia ya Church of England, ukibeba matumaini mapya lakini pia changamoto kubwa zinazohitaji uongozi wa busara, uwazi na maamuzi yenye usawa ndani ya kanisa na jamii pana ya waumini duniani.