Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma kielimu, baada ya kuanzisha programu maalum ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalumu, hususani wasio na uwezo wa kusikia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk Aneth Komba amesema wamehitimisha kikao kazi cha siku nne kilicholenga kupitia maudhui ya mtaala wa somo la hisabati kwa madarasa ya awali ili yaendane na mahitaji ya watoto viziwi.
“Nimekuja hapa kuhitimisha kikao kazi ambacho tumekaa kwa takribani siku nne, tukifanya kazi ya kupitia maudhui ya mtaala wa hisabati kwa darasa la kwanza hadi la tatu, ili kuangalia namna yatakavyowafikia watoto wenye uhitaji maalum, hususan viziwi,” amesema Dk Komba.
Amefafanua kuwa juhudi hizo zinaenda sambamba na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuboresha elimu, unaolenga kuhakikisha wanafunzi wanapata stadi muhimu za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) katika hatua za awali za elimu yao.
Dk Komba amesema taasisi hiyo imeingia ubia na Jenga Hub kubuni njia za kisasa za kufundishia, ikiwemo matumizi ya teknolojia, ambapo kwa sasa wameanza na kuboresha ujifunzaji wa hisabati kwa watoto wenye mahitaji maalum.
“Lengo ni kuhakikisha watoto hawa wanapata vifaa rafiki vya kujifunzia. Ndiyo maana tupo hapa ‘Kalimani App’, programu hii itasaidia watoto kujifunza kuhesabu. Tunaamini wakifika darasa la tatu watakuwa wamefikia malengo ya serikali ya kuwa na stadi hizi muhimu,” amesema.
Ameongeza kuwa maboresho ya sera ya elimu yameweka mkazo kwenye ujumuishi, hivyo hakuna mtoto anayepaswa kubaki nyuma kutokana na changamoto zozote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jenga Hub, Nancy Abraham Sumari amesema ‘Kalimani App’ imebuniwa mahususi kwa ajili ya watoto wenye changamoto ya usikivu ili kuwawezesha kujifunza kwa urahisi zaidi katika hatua za awali.
“Aplikesheni hii imelenga kumsaidia mtoto kiziwi au mwenye usikivu hafifu katika safari yake ya elimu, hasa elimu ya awali. Wiki hii tumekuwa na kikao kazi cha kuandaa maudhui kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ili kumsaidia mtoto kumudu somo la hisabati,” amesema Nancy.
Ameeleza kuwa ushirikiano walioupata kutoka kwa wataalamu wa elimu umekuwa chachu ya mafanikio ya mradi huo, huku akisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona kila mtoto anapata fursa sawa ya kujifunza.
“Shauku yetu kubwa ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebaki nyuma na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba aplikesheni hii itakuwa bure kwa watumiaji,” ameongeza.
Naye mwalimu, Faustina Msaki amesema ubunifu huo ni hatua muhimu katika kuleta usawa wa kielimu, akibainisha kuwa kwa muda mrefu watoto wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakikosa nyenzo rafiki za kujifunzia.
“Ukiangalia vipindi vingi vya watoto kwenye televisheni, vinalenga zaidi wale wanaosikia. Hivyo naamini mbinu hii itakuwa msaada mkubwa kwa watoto wenye changamoto ya kusikia na itakuwa njia bora ya kujifunza kwao,” amesema Msaki.