CRDB yawatahadharisha wajasiriamali dhidi ya mikopo hatarishi

Dar es Salaam. Wakati wajasiriamali wadogo hususan wanawake wanaouza mbogamboga na matunda wakizidi kuingia kwenye mikopo ili kukuza biashara zao, wamehimizwa kuchukua mikopo kwa malengo maalumu na kuepuka mikopo hatarishi inayoweza kuwaingiza katika mzigo wa madeni.

Wito huo umetolewa na CRDB Foundation wakati wa warsha ya mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wafanyabiashara wa mbogamboga iliyofanyika leo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja wa Elimu na Usimamizi wa CRDB Foundation, Joshua Mwakalobo amesema wajasiriamali wengi wadogo wamekuwa wakikopa fedha bila kuwa na mpango wa wazi wa matumizi, hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kurejesha mikopo na kuingia katika matatizo ya kifedha.

Amesema mkopo unapaswa kuwa nyenzo ya kukuza biashara na si chanzo cha mzigo wa madeni kwa mjasiriamali.

“Tunamzungumzia mama mbogamboga ambaye mara nyingi anahitaji mkopo ili kuongeza mtaji. Lakini kabla ya kuchukua mkopo ni muhimu kujiuliza kwanza, ninakopa kwa sababu gani na fedha hiyo itanisaidia vipi kukuza biashara yangu,” amesema Mwakalobo.

Mkurugenzi wa Tamwa Dk Rose Reuben akizungumza wakati wa warsha iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na CRDB Foundation kutoa elimu ya ujasiriamali na fedha kwa wanawake wauza mbogamboga.

Ameongeza kuwa baadhi ya wajasiriamali hukimbilia kukopa kwa sababu ya riba ndogo bila kuwa na mipango madhubuti wa matumizi ya fedha hizo.

“Cha muhimu ni kukopa kwa ajili ya kuongeza mtaji wa biashara na si kukopa kwa sababu tu mkopo una riba ndogo. Lazima kuwe na malengo ya wazi ya matumizi ya mkopo,” amesema.

Mwakalobo amesema changamoto kubwa inayowakabili wanawake wengi katika kupata mikopo ni kukosa dhamana, hali inayotokana na ukweli kwamba mali nyingi kama ardhi zinamilikiwa na wanaume.

Amesema ili kusaidia kundi hilo, CRDB Foundation imeanzisha programu zinazowasaidia wajasiriamali wadogo kupata mikopo hata kama hawana baadhi ya vigezo vya kawaida vinavyohitajika na taasisi za kifedha.

“Tumekuwa tukitoa msaada kwa wajasiriamali wadogo hata kama hawana vigezo kama TIN au leseni. Lengo ni kuwashika mkono ili waweze kukuza biashara zao na kujitegemea kiuchumi,” amesema.

Warsha hiyo iliandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na CRDB Foundation, ikiwa na lengo la kuwatambua na kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na biashara ya mbogamboga na matunda.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Tamwa, Dk Rose Reuben amesema taasisi hiyo inatambua mchango mkubwa wa wanawake wajasiriamali wadogo katika kukuza uchumi wa familia na jamii.

Amesema licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, wanawake wengi wameendelea kuonyesha uthubutu kwa kuanzisha na kuendesha biashara ndogo ndogo ili kujikwamua kiuchumi.

“Tamwa kwa kushirikiana na CRDB Foundation tunatambua na kuthamini juhudi za wanawake wajasiriamali wadogo wa mboga na matunda ambao kila siku wanapambana kuboresha maisha yao na ya familia zao,” amesema Dk Rose.

Amesema kuwatambua wanawake hao ni hatua muhimu ya kuibua fursa, changamoto na suluhisho litakalosaidia kuinua uchumi wao.

Baadhi ya wanawake wanaojihusisha na ujasiriamali wa kuuza mbogamboga wakisiliza mada wakati wa warsha iliyoandaliwa na Tamwa na CRDB Foundation kwa kundi hilo.

Dk Rose amebainisha kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, huku ikiendelea kupigania haki zao na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia biashara ndogo ndogo kama za mbogamboga ni moja ya njia muhimu za kuimarisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.