Kutenganishwa mifumo ya Ukimwi, NCDs kunavyoongeza magonjwa hayo Afrika

Unguja. Licha ya mafanikio yanayoonekana katika sekta ya afya hususani katika udhibiti wa ugonjwa wa Ukimwi Afrika, hatua hizo zinakabiliwa na changamoto ya kasi ya kuongezeka kwa magonjwa yasiyoyakuambukiza katika bara hiyo.

Watu wanaoishi na VVU wanapokuwa wazee wanakumbwa na magonjwa kama vile ya moyo, saratani, kisukari na magonjwa sugu ya mapafu, ambapo inakadiriwa hadi asilimia 44 ya wanaoishi na VVU pia wana NCD.

Hayo yamebainisha leo Machi 27, 2026 wakati wa uzinduzi wa programu ya Spark-NCD na huduma jumuishi za Ukimwi na NCD barani Afrika inayolenga kutengeneza na kusambaza ushahidi jinsi huduma hizi mbili ziweze kufanyiwa kazi pamoja.

Kutokana na hali hiyo, mkutano huo umewaleta pamoja watunga sera, wanasayansi, wataalamu wa utoaji huduma, sauti za wagonjwa na washirika kuzungumzia changamoto moja ya dharura inayofafanua mustakabali wa Afrika ambapo nchi hizo zimetakiwa kuunganisha mifumo kukabilina na magonjwa hayo.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alipomwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Afrika inashuhudia maendeleo mazuri katika matokeo ya afya, matarajio ya kuishi yamepanda kutoka takriban miaka 50 mwaka 2000 hadi miaka 63 sasa, yakielekea kufikia miaka 70 ifikapo 2050.

“Lakini pamoja na maendeleo haya, magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi, karibu milioni mbili ya Waafrika hupoteza maisha kila mwaka kutokana na shinikizo la damu na kisukari pekee. Hii inafanya Afrika kuwa na mzigo mkubwa wa magonjwa sugu duniani, jambo linalohitaji hatua za haraka na zilizoratibiwa,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema miaka 30 iliyopita Afrika ilikabiliana na janga la Ukimwi, kwa uongozi na ushirikiano, na kulibadilisha kuwa hali inayoweza kudhibitiwa “lakini leo huduma za Ukimwi na NCD bado zimegawanyika jambo lisilo endelevu.

Amesema utafiti wa miaka ya hivi karibuni nchini Tanzania na Uganda umeonyesha kuwa uunganishaji wa huduma za Ukimwi, kisukari na shinikizo la damu ni salama na unafuu wa gharama, na huboresha matokeo bila kuathiri Ukimwi hivyo wanahitaji mifumo inayomjali binadamu kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Afrika CDC, Dk Raji Tajudeen, Naibu Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kukuza magonjwa Afrika, Mohammed Abdulazizi amesema katika mpango mpya wa kimkakati wa Africa CDC, wamejumuisha mifumo jumuishi ya afya kwa ajili ya kinga na udhibiti wa magonjwa yenye mzigo mkubwa kwasababu nchi nyingi za Afrika ziko katika mpito wa milipuko wa magonjwa.

“Ufuatiliaji, kinga na huduma jumuishi za magonjwa sugu lazima ziwe nguzo kuu ya usalama na utawala wetu wa kiafya, kama ilivyokubaliwa hivi karibuni katika mkutano wa AU,”

Pia amesema Afrika inapaswa kuwa tayari kujenga mifumo, nguvu kazi, data na msukumo wa kisiasa unaohitajika kujibu kwa dharura, kwa ukubwa na kwa uongozi.

Amesema wakati magonjwa ya kuambukiza bado ni changamoto, magonjwa yasiyoambukiza hasa shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, saratani, magonjwa sugu ya mapafu na matatizo ya afya ya akili yanaongezeka kwa kasi katika kila kanda.

“Hali hii haibadili tu ni nani anaugua na kufa, bali inabadili mahitaji yanayowekwa kwenye mifumo yetu ya afya, uchumi na jamii,” amesema

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, “Hili si tatizo la baadaye. Ni ukweli uliopo sasa. NCD zinawagusa watu walio katika kilele cha maisha yao, zinasababisha ulemavu, zinapelekea umasikini wa kaya, kupunguza tija, na kuweka shinikizo endelevu kwenye mifumo ya afya ambayo haikubuniwa awali kushughulikia magonjwa sugu ya maisha yote kwa wingi.”

Amewataka washiriki hao katika mataifa yao kuimarisha umiliki wa kitaifa wa NCD, ufuatiliaji na huduma jumuishi za magonjwa sugu, kuwekeza katika mifumo itakayodumu na kuweka NCD katikati ya mipango ya afya ya umma.

“Kwa taasisi za afya ya umma na viongozi wa kiufundi, tujenge ushahidi unaosaidia sera. Kwa watafiti na vyuo, tuzalishe ushahidi wa utekelezaji unaofaa sera na unaoendana na hali halisi za Afrika. Kwa washirika na wafadhili, SPARK si uwekezaji wa muda mfupi bali ni fursa ya kimkakati ya kujenga uimara wa mifumo ya afya barani,” amesema na kuongeza

“Kwa jamii za kiraia na wagonjwa, sauti zenu ni muhimu, hatuwezi kujenga mifumo bila uzoefu wenu. Uzinduzi huu ukumbukwe si tu kama mwanzo wa programu, bali kama kuimarisha harakati za bara la kujenga mustakabali mzuri, wenye ustahimilivu na afya kwa watu wetu.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Tanzania, Dk Grace Magembe, Profesa Said Aboud kutoka NIMR amesema kwa zaidi ya miaka 40 wamepambana na Ukimwi na kwasasa Watanzania milioni moja wanaoishi na VVU wanaishi maisha marefu.

“Lakini jamii zetu sasa zinakabiliwa na changamoto mpya ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza yanayowakumba watu katika maisha yao ambapo zaidi ya theluthi moja ya vifo nchini, na yanayoongoza katika maradhi.

Amesema takriban robo mbili ya watu wenye NCD wana hatari ya kuingia katika umasikini kutokana na gharama za matibabu, na zaidi ya asilimia 75 ya wale wenye ugonjwa sugu wa figo wanakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na kijamii.

“Watu wanaoishi na VVU wanapokuwa wazee wanakumbwa na magonjwa kama vile ya moyo, saratani, kisukari na magonjwa sugu ya mapafu, inakadiriwa hadi asilimia 44 ya wanaoishi na VVU pia wana NCD,” amesema

Amesema mifumo ya afya bado inagawanyika, Ukimwi ukiendeshwa pekee na NCD ikikosekana katika huduma za msingi, hivyo uunganishaji si tena hiari, bali ni lazima.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Afya Uganda, Robert Mutumba amesema ni tamko la bara kwamba Afrika iko tayari kukabiliana na mzigo wa maradhi hayo kwa mikakati jumuishi, inayotokana na ushahidi na inayoweka mtu katikati.

Barani Afrika, tumeshuhudia mabadiliko ya kiafya na maambukizi mapya yamepungua, lakini mafanikio yameleta changamoto mpya: watu wanaoishi na VVU sasa wanaishi muda mrefu na wanakumbana na shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, mfadhaiko na saratani.

Amesema utafiti wa mwaka 2023 unaonyesha shinikizo la damu katika watu wazima ni 22, lakini miongoni mwa wanaoishi na VVU linatofautiana kati ya asilimia 24 hadi 37.

“Utafiti wa 2024 ulionyesha asilimia 13 ya wagonjwa kwenye matibabu ya Deltograva wana kiwango kilichopanda cha sukari. Vifo visivyohusiana na Ukimwi vinaongezeka miongoni mwa wale wanaotibiwa. Hivyo mifumo yetu iliyojikita kwenye maradhi ya aina moja inahitaji kubadilika,” amesema

Naye Kaimu Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Dk Saada Mkuya amesema Zanzibar, kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imepiga hatua kwa ubia wa umma na binafsi kwa kuboresha hospitali, mafunzo ya wafanyakazi na kuunganisha uchunguzi wa NCD na VVU katika huduma za msingi.

“Lakini changamoto bado ni kubwa, NCD zinachangia zaidi ya asilimia 30 ya vifo, zikiathiri vijana na nguvu kazi,” amesema