Simulizi ya Mhagama na magumu anayopitia

Mbeya. Mlemavu Ernest Mhagama (62), mkazi wa Mtaa wa Iganjo, Jiji la Mbeya, ametaja ukata wa kiuchumi kuwa chanzo cha mateso makali baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari miaka 19 sasa.

Hatua hiyo imemfanya kushindwa kufanya shughuli zozote za kiuchumi, licha ya miaka kadhaa iliyopita kuwa fundi maarufu wa kushona viatu na nguo katika mitaa mbalimbali mkoani hapa.

Leo, Machi 27, 2026, amekuwa miongoni mwa wanufaika wa msaada wa chakula kilichotolewa na Taasisi ya Tulia Trust kupitia “Bendera ya Upendo,” yenye lengo la kuibua wananchi waishio katika mazingira magumu.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mhagama amesema anapata mateso makubwa kwa kukosa fedha za kununua kifaa maalumu cha kupima sukari na dawa, jambo ambalo linapelekea kuwa na hali mbaya pindi ugonjwa huo ukipanda.

“Kimsingi, maisha yangu ni ya mateso makubwa. Kuna wakati kisukari kikipanda nashindwa kuamka na hata kukosa mahitaji muhimu kama chakula kwa wakati, kufuatia kuwa tegemeo kwenye familia ya mke na watoto wawili,” Amesema.

Mlemavu Ernest Mhagama (62).

Amesema kutokana na hali hiyo, ili kuiepuka mateso anayo yapitia na kugeuka omba omba, ameomba wadau hususan Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson, kumsaidia kwa pikipiki ya mataili matatu (bajaji), ili kuanzisha mradi wa kitega uchumi na kumudu maisha ya kila siku, hususan matibabu.

“Ugonjwa pasipo pesa huongezeka, lakini nikiseme kila dawa zikiisha niombe kwa wasamaria wema. Utafika wakati watanichoka. Ombi langu kubwa ni kwa Dk Tulia na wadau wengine kupata bajaji ili kufanya mradi wa kiuchumi,” Amesema.

Mhagama amesema mwaka 2005, aliwahi kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (CCM), mpaka mwaka 2022 ambapo aliachia kijiti, na sasa ni mjumbe wa jumuiya ya wazazi Kata ya Iganjo.

“Kipindi cha Rais Jakaya Kikwete nilikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (CCM), nikiwakilisha Mkoa wa Mbeya. Nimekutumikia kwa moyo mmoja na bado CCM, damu,” Amesema.

Awali, Mratibu na Kiongozi wa Mbio za Bendera ya Upendo, Daud Mwangosi, amesema kwa kipindi cha siku saba wamebaini kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye jamii, hususan kundi la wazee kukosa mahitaji muhimu.

“Tumewafikia wahitaji zaidi ya 1,000, lakini tumebaini changamoto kubwa sana ya wahitaji, wakiwemo wazee, walemavu na yatima, jambo ambalo tunaomba jamii kuwa na moyo wa kusaidia makundi hayo,” Amesema.

Washiriki wa mbio za Bendera ya Upendo wakiwa  Kata ya Iganjo Jiji la Mbeya  kabla ya kukabidhi chakula kwa wahitaji. Picha na Hawa Mathias

Amesema kupitia mbio hizo kila mlengwa amepewa kilo kumi za mchele kwa ajili ya kurejesha tabasamu la kusherehekea Sikukuu ya Pasaka mwezi ujao.

Naye, mkazi wa Kata ya Iganjo, Jiji la Mbeya, Ray James, amesema hilo ni darasa kwa jamii kutafakari nafasi ya kugusa wahitaji na kutoa mahitaji mbalimbali, hususan chakula, mavazi na makazi.

Mbio za Bendera ya Upendo zimekimbizwa mitaa 61, Kata 13, katika Jimbo la Uyole kama sehemu ya kutimiza miaka 10 ya Taasisi ya Tulia Trust.