SIMBA inaweza kuchagua kiwanja chochote inachotaka kisha ikashinda lakini kuna viwili haitaki kabisa kuvisikia sasa Azam imeshtukia kitu na kuwapeleka wekundu hao kwenye kimoja kati ya hivyo viwili kattika mchezo wao ujao.
Mchezo wa kwanza wa Simba dhidi ya Azam msimu huu ulipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Desemba 7,2025 na Simba kuchapwa mabao 2-0 ukiwa ndio mchezo pekee walioangusha pointi zote tatu mpaka sasa.
Azam ikiwa inajiandaa kurudiana na wekundu hao imefanya maamuzi haraka na kuamua kuwa mchezo wao wa marudio upigwe kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Baada ya ligi kurejea Matajiri wa Chamazi wataanza kuvaana na Singida Black Stars, Aprili Mosi katika Uwanja wa Airtel, Singida akili zitaanza kujipanga kukutana na Simba mchezo ambao utapigwa Aprili 5, 2026, Uwanja wa Azam Complex.
Ofisa Habari wa Azam Thabit Zacharia ‘Zaka Zakazi’ ameliambia Mwanaspoti kwamba tayari uongozi wao ulishaijulisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) juu ya mabadiliko ya uwanja wa mchezo huo kupigwa Azam Complex. “Nikweli huo mchezo utachezwa Azam Complex, hilo lilishafanyika maamuzi yake na bodi ilishajulishwa kwasasa tunaendelea na maandalizi ya mchezo wetu unaofuata dhidi ya Singida tukimaliza hapo tutakuwa na hesabu za kukutana na Simba,” amesema Zaka.
Simba na Azam uwanjani Azam Complex takwimu zinaonyesha zimekutana mara tatu ambapo mechi zote zikimalizika kwa suluhu huku mbili zikiisha kwa sare ya 1-1.
Mwanaspoti linafahamu kuwa maamuzi ya mwisho ya mabadiliko ya uwanja huo yalisukumwa zaidi na kocha wa Azam, Florent Ibenge, ambaye ametaka timu yake icheze mechi hizo kubwa kwenye uwanja wake badala ya uwanja mwingine.
“Tulikuwa tunafikiria kutafuta uwanja wa mchezo huo lakini Ibenge akatuhoji tunakimbia kitu gani kucheza hapa Azam,akasema anataka timu yake icheze hapa hapa na sio uwanja mwingine ili ijivunie faida ya kucheza nyumbani,” amesema bosi huyo wa juu wa Azam FC.
