Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ili Tanzania ifikie uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 kama ilivyobainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo (Dira 2050), inahitaji ukuaji endelevu wa pato la taifa wa angalau asilimia 10 kila mwaka kuanzia 2026 hadi 2050.
Rais Mwinyi amebainisha hayo leo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa uhakiki wa rasimu ya mpango wa pili wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji (Mkumbi II).
Mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikiirudisha nyuma nchi hii.
Hata hivyo, wadau wamebainisha changamoto kadhaa ambazo wangependa kuona zinafanyiwa kazi kwenye Mkumbi II, miongoni mwazo ni utitiri wa kodi na tozo pamoja na uwepo wa mamlaka nyingi zinazokusanya mapato hayo.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Rais Mwinyi amesema Dira 2050 inalenga kufikia uchumi wenye thamani ya dola trilioni 1 pamoja na kipato cha kila mtu cha wastani wa takribani dola 7,000 (sawa na takribani Sh18.2 milioni).
Amesema kwa muktadha huo, sekta binafsi imeainishwa kuwa kiungo muhimu na injini ya kufanikisha malengo hayo ya maendeleo.
“Ili kufikia azma hiyo, nchi inahitaji ukuaji endelevu wa pato la taifa wa angalau asilimia 10 kwa mwaka kuanzia 2026 hadi 2050. Hii inahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji, viwanda, kilimo cha kisasa, uchumi wa buluu, nishati, Tehama, pamoja na huduma zenye tija na thamani kubwa,” amesema.
Amesisitiza kwamba Serikali pekee haiwezi kufanikisha malengo haya. Hivyo, ushiriki mpana wa sekta binafsi kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa na huduma ni jambo lililopewa uzito na kuwekewa msisitizo mkubwa katika Dira 2050.
“Sekta binafsi haitarajiwi kutoa mchango kwa serikali bali itatoa mchango katika ukuzaji wa uchumi kupitia uwekezaji wenye tija katika sekta mbalimbali. Uwekezaji huo unatarajiwa si tu kuipa faida sekta binafsi kupitia faida ya uwekezaji, bali pia kutoa ajira kwa wananchi wakiwemo vijana,” amesema.
Rais Mwinyi amesisitiza kuwa: “Utekelezaji wa ajenda hizi unategemea kwa kiasi kikubwa urahisi na ubora wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara katika ngazi zote.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo amesema lengo kubwa la kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni kutoka kuwa wadhibiti na kuwa wawezeshaji.
Pia, amesema inalenga kuondoka kwenye hali ya kutiliana shaka kati ya Serikali na sekta binafsi na kujenga imani isiyo na shaka kati ya wadau hao muhimu katika kuchagiza maendeleo ya taifa.
“Hili ni jambo kubwa linalohitaji mabadiliko ya mtazamo. Taasisi zetu zinatakiwa kutambua kwamba zina jukumu la kuiwezesha sekta binafsi na siyo kuwa wadhibiti pekee,” amesema Profesa Kitila.
Ameongeza kuwa rasimu hiyo inaangazia maeneo 246 yanayohitaji hatua za mageuzi ili kuondoa vikwazo vinavyotajwa kwa kiasi kikubwa kuwa changamoto kuu kwa wajasiriamali nchini kote.
“Bado kuna hali ya kulaumiana: sekta binafsi inaona serikali haijatengeneza mazingira rafiki kwa biashara, huku baadhi ya taasisi za umma zikiwaona kama wakwepa kodi. Ukosefu huu wa imani unapaswa kushughulikiwa, na Mkumbi II inapaswa kuhakikisha hilo,” ameeleza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Juliana Pallangyo amesisitiza nafasi muhimu ya sekta binafsi katika mageuzi ya kiuchumi ya nchi, akibainisha kuwa inatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 katika kufikia Dira 2050.
Amesema Mkumbi I ilipunguza kodi nyingi, lakini amesisitiza kuwa bado kuna kazi zaidi ya kufanya ili kuimarisha mazingira ya sekta binafsi.
“Ingawa kumekuwa na maboresho makubwa, sekta binafsi inatambua jitihada za serikali na ina matumaini kuwa Mkumbi II italeta maboresho makubwa zaidi katika mazingira ya biashara na uwekezaji,” amesema.
Licha ya maendeleo hayo, changamoto kadhaa bado zipo. Miongoni mwazo ni umuhimu wa sekta binafsi kushirikishwa kikamilifu kama mdau badala ya kuwa mtazamaji.
Aidha, tofauti za kanuni na taratibu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara zinaendelea kuleta vikwazo kwa uendeshaji mzuri wa biashara. Mkumbi II inalenga kuoanisha kanuni hizo na kuimarisha ushirikiano ili kuunda mazingira bora zaidi ya biashara.
“Sisi kama sekta binafsi tutaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha ukuaji wa uchumi na kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo 2050, ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea mchango wa sekta binafsi wa zaidi ya asilimia 70,” amesisitiza mwakilishi huyo wa TPSF.
