Bunda. Mbio za urais mwaka 2030 ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeanza kufukuta ndani ya chama hicho huku Stephen Wasira akiwoanya wale wote walioanza harakati hizo muda haujafika.
Wasira ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara amesema wale wote wanaofanya hivyo wanakiuka kanuni, miongozo na utaratibu na hatua hiyo inaweza kukigawa chama badala ya kukijenga hivyo inapaswa kukemewa.
Mwanasiasa huyo mkongwe anatao kauli hiyo takribani miezi minne kupita tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uliomweka madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, mwakani 2027, chama hicho tawala-CCM kitafanya uchaguzi wake kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa hali inayozidisha joto la uchaguzi mkuu huo wa mwaka 2030.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais Samia huu ni muhala wake wa mwisho na uchaguzi ujao utakaofanyika miaka minne ijayo, hatoshiriki.
Leo Ijumaa, Machi 27, 2026, Wasira akiwa Mjini Bunda, Mkoa wa Mara alipokuwa akiweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la ofisi za CCM Wilaya ya Bunda ambazo zilichomwa moto katika na vurugu za Oktoba 29, 2025 amezungumzia mbio hizo za urais.
Amesema ndani ya chama kuna kundi la wanachama ambao hawana kazi za msingi ndani ya CCM zaidi ya kujihusisha na makundi ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Wasira, kundi hilo limeanza kujipanga kwa kuunda safu kuanzia ngazi za kata, hali ambayo inaweza kusababisha mgawanyiko ndani ya CCM kwa kuwa kila mmoja anataka kuwa na wafuasi wake badala ya kuimarisha umoja.
“Leo unasikia kila mtu anataka kuwa na watu wake wa kata, anaunda safu yake. Sasa tukiruhusu kila mmoja awe na kundi lake, CCM itabaki wapi? Tunahitaji kuwa chama kimoja chenye mshikamano, si makundi ya watu binafsi,” amesema.
Amesisitiza wanachama wanapaswa kuacha kuzungumzia urais wa 2030, badala yake wajikite katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kujenga upya misingi imara ya kisiasa kuelekea uchaguzi ujazo.
Ameeleza taifa bado lina kazi kubwa ya maendeleo inayohitaji umoja na mshikamano wa kisiasa.
Wasira alihoji uhalali wa baadhi ya watu kuanza kujitangaza mapema kuwania urais wa 2030, akisema hakuna anayeweza kujihakikishia uwepo wake hadi wakati huo.
“Unazungumziaje urais wa 2030 leo, wakati hata hujui kama utakuwepo? Hiyo ni kama kumjaribu Mungu. Wakati huu tunapaswa kujikita kwenye kazi za kujenga Chama na nchi,” alisisitiza.
Aidha, alionya tabia ya baadhi ya watu kutumia fedha kushawishi wanachama maskini kuungwa mkono, akieleza kuwa hali hiyo ni hatari na inaweza kuharibu maadili ya Chama. Amesema baadhi ya watu wanatumia udhaifu wa kiuchumi wa wanachama kama mtaji wa kisiasa, jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
Katika hatua nyingine, Wassira alirejea matukio ya vurugu za Oktoba 29, mwaka jana ambapo baadhi ya watu walichoma ofisi za Chama, wakidhani wanaweza kuidhoofisha CCM.
Amesema chama hakiwezi kuangamizwa kwa vitendo vya aina hiyo kwa kuwa kina wanachama zaidi ya milioni 13 nchi nzima.
“CCM haiwezi kuchomwa moto ikaisha. Ni chama cha watu milioni 13, huwezi kukimaliza kwa kuchoma jengo. Ukifanya hivyo, sisi tunasema asanteni, tutajenga upya na kuwa imara zaidi,” amesema.
Ameongeza nguvu ya chama hicho iko kwa wanachama wake na historia yake, akisisitiza kuwa lengo kuu kwa sasa ni kuhakikisha chama kinabaki imara, kinajenga mshikamano na kinajiandaa vizuri kwa chaguzi zijazo ili kuendelea kuongoza nchi kwa mafanikio.
