Mashindano ya Asma Mwinyi Next Generation kuanza Jumamosi

TIMU 20 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, zinatarajiwa kushiriki michuano ya Afrika ya mchezo wa mpira wa kikapu kwa vijana yanayoanza kesho Jumamosi Machi 28, 2026.

Mashindano hayo yanayofahamika kwa jina la Asma Mwinyi Next Generation, yatafanyika kwa siku tatu kwenye uwanja wa ndani wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Timu kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Tanzania Bara na Afrika Kusini, zitashiriki mashindano hayo huku mwenyeji akiwa Zanzibar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa michuano hiyo, Issa Chiwile, amesema maandalizi yote yamekamilika na timu zimeanza kuwasili Zanzibar tayari kwa kushindania ubingwa.

Amesema, lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji vya vijana na kuwapa uzoefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa mapema, jambo ambalo litasaidia kukuza kiwango cha mchezo huo katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla.

Chiwile amongezea kuwa, mashindano hayo yatatoa fursa kwa makocha na wadau wa mchezo huo kubadilishana uzoefu pamoja na kutambua vipaji vipya vitakavyoweza kuendelezwa katika timu mbalimbali za baadaye.

Aidha aliwataka wananchi na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kufuatilia mashindano hayo ili kuwapa hamasa vijana wanaoshiriki na kuendeleza maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu visiwani Zanzibar. 

Michuano hiyo itawakutanisha vijana wenye umri kuanzia miaka 13 hadi 18, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza vipaji vya mchezo wa mpira wa kikapu barani Afrika na kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika ngazi ya kimataifa.