Mwanamuziki wa zamani wa Hip Hop aliyegeukia siasa, Balen Shah, ameapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Nepal kufuatia ushindi mkubwa wa chama chake katika uchaguzi wa bunge.
Shah amekabidhiwa jukumu hilo leo, Ijumaa, Machi 27, 2026, huku akipewa wajibu wa kurejesha utulivu wa kisiasa na kuchochea ajira nchini humo.
Shah (35), ambaye pia aliwahi kuwa meya wa Kathmandu, anaingia madarakani akiwa Waziri Mkuu mdogo zaidi kwa miongo kadhaa, na wa kwanza kutoka jamii ya Madhesi kushika wadhifa huo.
Chama chake cha Rastriya Swatantra kilishinda viti 182 kati ya 275 katika uchaguzi uliofanyika Machi 5 mwaka huu.
Kiongozi huyo ameapishwa leo na Rais, Ram Chandra Paudel, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Kathmandu, iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali na wanadiplomasia, huku makuhani wa dini za Kihindu na Kibudha wakiongoza maombi ya amani.
Mara baada ya kuapishwa, Shah ametangaza baraza lake la mawaziri lenye wajumbe 14, akitimiza ahadi yake ya kuunda serikali ndogo ili kupunguza matumizi ya umma.
Katika uteuzi huo wa baraza hilo, amemteua mwanauchumi Swarnim Wagle kuwa Waziri wa Fedha.
Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo mpya anakabiliwa na mtihani wa kushughulikia athari za maandamano ya mwaka 2025 yaliyosababisha vifo vya watu 76, pamoja na kuhakikisha uwajibikaji kwa waliotajwa kuhusika, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Sharma Oli.
Kwa muda mrefu, Nepal imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa, ikiwa na zaidi ya serikali 30 tangu mwaka 1990 bila hata moja kukamilisha muhula wake wa miaka mitano, hali inayochangia kuendelea kwa changamoto za umaskini na ukosefu wa ajira kwa wananchi wake.
