Dar es Salaam. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Zahra Maruma amesema kuboreshwa kwa mifumo ya kisheria na kisera itakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) kutachangia kujenga jamii yenye misingi imara na ustawi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Machi 27, 2026, akiwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa wiki ya kongamano la Njia Mbadala za Utatuzi wa Migogoro, Jaji Maruma, aliyemwakilisha Wakili Mkuu wa Serikali, amesema ukosefu wa maboresho katika mifumo hiyo umechangia kuwepo kwa pengo kubwa la ushiriki wa wanawake ikilinganishwa na wanaume wanaoshika nafasi nyingi za uamuzi.
“Wanawake ni wazuri katika usuluhishi kwa sababu ni wavumilivu na wasikivu; tukiboresha mifumo ya kisheria na kisera, wataweza kutumia fursa zilizopo na kusaidia kujenga jamii yenye misingi imara na ustawi,” amesema Jaji Maruma.
Amesema hatua hiyo ya maboresho haitawanufaisha wanawake pekee, bali pia ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2025/2050, inayolenga kuimarisha usawa wa kijinsia nchini.
Kwa mujibu wake, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ni rafiki zaidi kuliko mfumo wa kawaida wa mahakamani, kwani huokoa muda, hupunguza gharama na kujenga maelewano.
“Migogoro inapojitokeza huacha nyufa katika jamii, lakini usuluhishi hujenga maelewano. Mwanamke akiwezeshwa ana nafasi kubwa ya kufanikisha hilo,” amesema.
Katikati ya maelezo yake, amesema Tanzania ina fursa ya kuwa kinara barani Afrika katika matumizi ya usuluhishi, akieleza kuwa takribani sheria 12 zinatambua na kuruhusu matumizi ya njia hizo.
“Mwaka 2025, zaidi ya mashauri 386 yalimalizwa kupitia usuluhishi mahakamani na zaidi ya mashauri 500 yakamalizwa nje ya mahakama kupitia mabaraza,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Laetitia Ntagazwa amesema chama hicho kimeanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Moja ya jukumu letu ni kulinda umma wa Watanzania. Kupitia kongamano hili tunalenga kuongeza ushiriki wa wanawake, kwani bado kuna pengo kubwa; Afrika, wanawake ni asilimia 28 tu katika sekta hii,” amesema Wakili Ntagazwa.
Amesema nchini Tanzania, wanawake waliothibitishwa kama wasuluhishi ni 82 pekee, ikilinganishwa na wanaume 444, hali inayoonyesha umuhimu wa kuongeza juhudi za kuwawezesha wanawake.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Kimataifa Cha Usuluhishi kwa Njia Mbadala, Wakili Godson Nyange amesema elimu, makongamano na ushirikiano kati ya serikali na wadau ni muhimu katika kuongeza ushiriki wa wanawake.
“Tumeandaa kongamano hili kuwajengea uwezo wanawake na kuujulisha umma kuhusu huduma za usuluhishi ili wananchi wenye changamoto wajitokeze kupata suluhisho,” amesema Godson Nyange.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usuluhishi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Saddy Sevingi amesema ofisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sekta hiyo kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu.
“Tuna kitengo maalumu cha usuluhishi na tunaendelea kushirikiana na wadau ili kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala,” amesema Sevingi.
Kongamano hilo linalojumuisha wataunga sera, wanasheria na viongozi wa biashara limeandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro Tanzania (TIAC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria litaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kutoka Majadiliano hadi Hatua: Kuendeleza Ushirikishwaji wa Wanawake katika Utatuzi Migogoro kwa Njia Mbadala”.
