Afya ya baba inavyoweza kuongeza hatari  kwa mjamzito

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu mjadala wa afya ya ujauzito umejikita zaidi kwa mama, huku baba akionekana kuchangia mbegu pekee.

Hata hivyo, kazi mpya za kitafiti zinaonyesha kuwa afya ya mwanaume kabla ya kutungisha mimba ina mchango mkubwa katika hatari na matokeo ya ujauzito.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2024 katika jarida la Cells uitwao: “The Bad Father: Paternal Role in Biology of Pregnancy and in Birth Outcome” unaeleza kuwa baba anaweza kuwa “baba mzuri au mbaya” kulingana na afya yake kabla ya mimba.

Watafiti wakiongozwa na Profesa Stefano Raffaele Giannubilo wanaeleza kuwa nusu ya vinasaba vya mtoto hutoka kwa baba, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa kondo la nyuma, mwitikio wa kinga ya mama na hatari ya matatizo kama shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito (preeclampsia), kujifungua kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa na uzito mdogo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mwanaume aliyewahi kusababisha ujauzito wenye tatizo la ‘preeclampsia’ ana uwezekano mara mbili wa kusababisha hali hiyo kwa mwanamke mwingine.

Utafiti mwingine uliochapishwa mwaka 2021 katika jarida la American Journal of Obstetrics & Gynecology MFM ulitumia takwimu za zaidi ya watoto 669,000 waliozaliwa kati ya  mwaka 2009 na  mwaka 2016 nchini Marekani.

Utafiti huo ulihusisha wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 45 wasio na magonjwa sugu kabla ya mimba, huku wenza wao wakifanyiwa tathmini ya afya.

Matokeo yanaonyesha kuwa wanawake ambao wenza wao walikuwa na magonjwa mawili au zaidi yanayohusiana na ‘metabolic syndrome’,  ikiwamo shinikizo la damu, kisukari na unene uliopitiliza,  walikuwa na ongezeko la asilimia 21 ya hatari ya ‘preeclampsia’ isiyo kali, ongezeko la asilimia 19 ya preeclampsia kali au degedege la mimba (eclampsia),

na ongezeko la asilimia tisa ya matatizo makubwa wakati au baada ya kujifungua.

Hata hivyo, kazi hizo za kitafiti hazikuonyesha tofauti kubwa katika matatizo ya kondo la nyuma kama placenta previa (kondo la nyuma kukaa chini sana kwenye mfuko wa uzazi na kufunika sehemu au mlango wa kizazi au placenta accrete |(kondo la nyuma kushikamana kwa nguvu sana na ukuta wa mfuko wa uzazi  kuliko kawaida).

Wataalamu wasema maandalizi yawahusu wote.

Mkufunzi wa elimu ya afya ya uzazi, Mgeni Kisesa, anasema msongo wa mawazo kwa mwanaume unaweza kuathiri ubora wa mbegu.

“Watu wengi hudhani msongo unatokana na kukosa fedha pekee, lakini hata wenye kipato kikubwa wanaweza kuwa na viwango vya juu vya stress vinavyoathiri afya ya uzazi,” anasema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu  cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Faithness Kiondo, anasema mwanaume anapaswa kuwa chanzo cha utulivu wa kihisia kwa mwenza wake.

“Mwanaume anaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kazi za nyumbani, kuhudhuria kliniki pamoja na mwenza wake na kujifunza kuhusu mabadiliko ya ujauzito ili kuelewa anachopitia,” anasema.

Wataalamu wanasema matokeo haya yanafungua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa huduma za afya kabla ya mimba kwa wanaume, eneo ambalo bado halijapewa kipaumbele katika mifumo mingi ya afya, ikiwamo Tanzania.

Tafiti zinaweka wazi kuwa maandalizi ya ujauzito si jukumu la mwanamke pekee. Afya ya baba kuanzia lishe bora, mazoezi, kuacha sigara na pombe hadi kudhibiti magonjwa sugu,  ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya ya mama na mtoto.

Kwa nchi zinazoendelea, wataalamu wanasema ipo haja ya kuanzisha elimu na huduma za afya ya uzazi zinazowahusisha wanaume kikamilifu, ili kupunguza vifo na matatizo ya uzazi yanayozuilika.