Tughe Morogoro yaomba watumishi wapya

Morogoro. Serikali imeombwa kuidhinisha vibali vya ajira mpya kwa Idara ya Uhamiaji nchini ili kuondoa changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali katika idara hiyo ikiwemo kada ya udereva.

Kada nyingine zenye upungufu wa watumishi ni uhasibu, wakaguzi wa ndani wa hesabu, watumishi sekta ya afya wakiwemo wauguzi na madaktari kwa ajili ya kituo cha afya kilichoanzishwa na idara hiyo cha Raphael Kubaga kilichopo jijini Tanga.

Kada nyingine ni watunza kumbukumbu na nyaraka na waandishi waendesha ofisi kwa ajili ya utendaji wa kazi za kila siku katika idara hiyo.

Ombi hilo limetolewa na Katibu wa Chama cha wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Tawi la Uhamiaji, Francis Katawa wakati akitoa taarifa kwenye mkutano mkuu wa Tughe tawi la uhamiaji ambapo ameeleza sababu za upungufu wa watumishi kwenye idara hiyo.

Baadhi ya sababu alizozitaja Katawa ni pamoja na watumishi kustaafu, kuhama na kwenda kufanya kazi katika taasisi nyingine na baadhi yao kufariki dunia.

Amesema changamoto hiyo ya upungufu wa watumishi imeshawasilishwa kwenye mamlaka mbalimbali za ajira na wana imani itafanyiwa kazi kwa kuwa idara ya uhamiaji ni taasisi inayofanya kazi kwa kuhusisha watumishi wa kada mbalimbali.

Awali, akifungua mkutano huo kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Anna Makakala, Naibu Kamishna wa Uhamiaji ambaye pia ni Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Elizabeth Lukuwi amesema Serikali kupitia mamlaka husika za ajira, inaendelea kutambua na kufanyia kazi changamoto hiyo.

Lukuwi amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi, mafanikio ya idara hiyo yanategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu, uadilifu na weledi wa watumishi wa kada mbalimbali zilizopo kwenye idara hiyo.

“Kupitia Tughe, niwahimize watumishi wenzangu kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na ubunifu katika utendaji wa kazi za kila siku, kila mmoja wenu anayo nafasi ya kuchangia maendeleo ya Taasisi hii pamoja na Taifa kwa ujumla,” amesema Lukuwi.

Amesema  vyama vya wafabyakazi ni nguzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa watumishi na kuleta uwiano mzuri kati ya wafanyakazi na mwajiri hivyo menejimenti  nzima ya Idara  ya Uhamiaji inathamini chama hicho pamoja na mchango wa kila mtumishi na hivyo ameahidi kushirikiana na chama pamoja na watumishi katika kuboresha mazingira ya kazi.