Mwanza. Wakati idadi ya watu wenye matatizo ya macho ikiendelea kuongezeka duniani, wataalamu wa afya wameibuka na tahadhari juu ya kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa glakoma (shinikizo la macho), unaotajwa kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya upofu wa kudumu.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kimataifa, ikiwemo utafiti wa Taasisi ya Ophthalmology ya Uingereza, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2060 zaidi ya watu milioni 1.6 wenye umri wa miaka 40 na kuendelea wanaweza kuathiriwa na ugonjwa huo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa glakoma ni miongoni mwa sababu kuu za upofu duniani.
Mwaka 2020, takribani watu milioni 76 waliishi na ugonjwa huo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya milioni 111 ifikapo mwaka 2040 endapo hatua za kinga na uchunguzi wa mapema hazitaimarishwa.
Kwa mujibu wa WHO, tangu mwaka 2002 glakoma imekuwa sababu ya pili kwa ukubwa ya upofu duniani, ikitanguliwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho (cataracts). Tofauti yake kubwa ni kwamba upofu unaosababishwa na glakoma hauwezi kurekebishwa, jambo linaloufanya uchunguzi wa mapema kuwa wa lazima.
Glakoma ni kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamu wa macho unaosafirisha taarifa za uoni kwenda kwenye ubongo. Mara nyingi husababishwa na kuongezeka kwa shinikizo ndani ya jicho.
Shinikizo hilo linapozidi kiwango cha kawaida, huanza kuharibu neva ya macho taratibu. Madhara yake ni kupungua kwa uwezo wa kuona hatua kwa hatua, na endapo haitagunduliwa mapema, mgonjwa anaweza kupoteza kabisa uwezo wa kuona.
Changamoto kubwa ya ugonjwa huu ni kwamba katika hatua za mwanzo hauna dalili. Tafiti zinaonyesha kuwa angalau asilimia 50 ya wagonjwa wa glakoma aina ya ‘open angle’ hawajui kama wana ugonjwa huo, kwa sababu huendelea polepole bila maumivu.
Wataalamu wanasema wengi hugundua wakiwa tayari wamepoteza sehemu kubwa ya uwezo wa kuona, hali inayofanya matibabu yawe ya kudhibiti tu, si kurejesha uoni.
Ingawa glakoma huonekana zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, hata walioanzia miaka 40 wanaweza kuanza kuathirika.
Makundi yaliyo katika hatari kubwa ni pamoja na wenye umri wa zaidi ya miaka 60, wenye historia ya ugonjwa huo katika familia, wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu na wenye magonjwa sugu au upungufu wa kinga mwilini.
Wengine ni waliowahi kupata jeraha la jicho, watoto wanaozaliwa na tatizo hilo na wanaotumia dawa za macho zenye steroidi kwa muda mrefu.
Dk Mdhamini Francis wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni (KDH) anasema historia ya kifamilia ni sababu muhimu kwa kuwa ugonjwa huo unaweza kurithiwa.
“Watu wenye umri mkubwa wako kwenye hatari zaidi. Aidha, wagonjwa wa kisukari, presha au wenye upungufu wa kinga wanapaswa kuchunguza macho mara kwa mara,” anasema.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, hadi mwaka 2019 inakadiriwa kuwa asilimia 4.2 ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40 nchini wana glakoma sawa na takribani watu 440,000.
Hata hivyo, kati ya asilimia 70 hadi 90 ya wagonjwa hao hawajui kama wana ugonjwa huo kutokana na ukosefu wa utamaduni wa kupima macho mara kwa mara.
Taarifa ya wizara hiyo inaeleza kuwa mwaka 2018 ni watu 18,000 pekee walioripotiwa kuhudhuria vituo vya tiba wakiwa na tatizo la shinikizo la macho, idadi ndogo ikilinganishwa na walioko kwenye hatari ambao bado hawajagunduliwa.
Wataalamu wanaonya kuwa kwa kuwa glakoma huleta ulemavu katika umri wa uzalishaji, taifa hupoteza nguvu kazi na kuongeza mzigo wa kiuchumi kwa familia na jamii.
Hakuna tiba, lakini inaweza kudhibitiwa
Kwa sasa, glakoma haina tiba ya kuponya kabisa. Hata hivyo, ikigundulika mapema, inaweza kudhibitiwa kwa dawa za kupunguza shinikizo la jicho, tiba ya kuboresha mtiririko wa maji ndani ya jicho na upasuaji maalum wa kupunguza presha ya jicho.
Wataalamu wanashauri watu wote wenye umri wa zaidi ya miaka 40 kupima macho angalau mara moja kila mwaka, hata kama hawana dalili zozote.
“Ili kugundua ugonjwa huu mapema, ni muhimu kupima macho angalau mara moja kila mwaka hasa kwa makundi yaliyo hatarini, hata kama mtu haoni tatizo lolote,” anasisitiza Dk Francis.
Kwa ujumla, glakoma anabaki kuwa adui mkimya wa macho huku madhara yake yakibaki makubwa na ya kudumu. Uchunguzi wa mapema ndio silaha kuu ya kuzuia upofu usiorekebishika.