Russia. Usonji kitabibu hujulikana kama Autism, ni dosari katika ukuaji wa ubongo ambayo ni sehemu ya mfumo wa Neva inayoathiri mawasiliano, mwingiliano wa kijamii na tabia.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO, usonji huathiri takribani mtoto mmoja kati ya 100 ulimwenguni kote. Watoto wa kiume wakiwa na uwezekano wa kugundilika mara nne zaidi ya watoto wa kike. Viashiria huwa wazi zaidi katika umri wa miaka miwili hadui mitatu.
Tatizo hili si ugonjwa, hakuna dawa ya kuponesha bali ni hitilafu ya kudumu ya upigaji hatua za ukuaji wa neva. Asilimia 40-80% ni tatizo linahusishwa na chembe za urithi, mazingira na sababu zingine hazijulikani.
Jamii zisizo na uelewa zimekuwa zikiwawahukumu watoto wenye tatizo hilo kama ni watoto wakaidi, watukutu au wajeuri, pasina kujua hali hizo ni kutokana ni athari za mfumo wa neva wenye dosari.
Ipo dhana potofu katika jamii wakihusisha tatizo hili na chanjo, kitu ambacho si kweli. Tatizo hili pia haliwezi kuchangiwa na wazazi na linajitokeza kwa yoyote yule kutoka tabaka lolote duniani.
Mara nyingi tatizo hili huweza kubainika kupitia historia kutoka kwa wazazi, walezi na uchunguzi wa wataalam wa afya kupitia ufuatiliaji wa ukuaji na tabia za watoto.
Watu wenye tatizo hili wanaweza kupata mkwamo au ugumu wa kubadili shughuli moja mpaka nyingine, na huwa na hisia kali ikiwamo unga’nga’nizi wa kila anachokifanya, uwezo mdogo kiakili na utambuzi na kufanya vitendo vya kujirudia.
Mara nyingi wanakumbana na hali zingine kama vile msongo wa mawazo, wasiwasi, kutotulia, matatizo ya usingizi na mfumo wa chakula. Asilimia 30-40% ya watu wenye usonji hupata tatizo la kifafa.
Watoto walioathirika huwa na mwingiliano mdogo au usio wa kawaida wa kijamii, ugumu na uhusiano wa rika. Hata wanapokuwa na wenzao hawaonyeshi shauku ya kujumuika.
Huchelewa kuzungumza, kuzungumza maneno yasiyoeleweka, kuzungumza kwa kujirudia rudia na kuwa na ugumu kujadili au kuongea ana kwa ana. Vile vile hushindwa kujifunza na kuelewa haraka mambo madogo madogo.
Huwa na kawaida ya kukomalia kufanya jambo fulani mara kwa mara, akionyesha kutotaka kuacha, hata ukimkataza hurudia na huwa wakali na kukasirika haraka.
Ni kawaida kupata hisia au msisimko wa fahamu uliokithiri au wa kiwango cha chini wa visisimuzi kama vile sauti, mwanga, mguso, mtetemo au maumivu.
Tatizo hili halina tiba ili kupona, bali wanahitaji huduma mbalimbali kama tiba ya lugha, ujuzi na kazi. Dawa zinaweza kutumika kukabiliana na madhara yanayombatana nayo ikiwamo kifafa, hofu kali na kukosa usingizi.
Uwezo na mahitaji ya watu wenye usonji hutofautiana sana, ambapo baadhi yao wanaweza kuishi kwa kujitegemea, huku wengine wakihitaji msaada kwa maisha yote.
