MABOSI wa Yanga wameshamaliza presha iliyokuwa kwenye benchi lao la ufundi wakiweka mambo sawa lakini kuna lingine limeanza kuwakumba mastaa wa timu hiyo wakishushiwa adhabu kali kwa makosa ya kimaadili.
Iko hivi, Yanga wana kanuni zao za maadili ambazo wafanyakazi wake wakiwamo wachezaji na makocha zinawataka kukaa mstari mmoja na ukienda kinyume tu hazikuachi salama, utakutana na adhabu kulingana na makosa uliyofanya.
Kilichowakuta baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kutoka timu kubwa na ile ya vijana hivi karibuni ni pale walipokaidi kusafiri na kikosi hicho hata kama ni majeruhi hasa wale wa muda mfupi ambapo waliofanya hivyo wamekutana na adhabu kali.
Bosi mmoja wa juu wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kuwa, uongozi wao upo makini kusimamia nidhamu kwa wachezaji ambapo mastaa wawili wa timu kubwa beki Chadrack Boka na mshambuliaji Aurelio Laurindo ‘Depu’ kukatwa fedha kutokana na makosa waliyofanya. Mastaa hao ambao ni majeruhi, walitakiwa kusafiri na kikosi licha ya kwamba ni majeruhi ambapo walitakiwa kuhudumiwa na madaktari wa Yanga ambao walisafiri na timu hiyo kwenda kwenye mechi dhidi ya TRA United jijini Arusha na dhidi ya Mtibwa Sugar iliyopigwa jijini Dodoma.
Mastaa hao wawili hawakusafiri na kikosi hicho ambapo kosa hilo kila mmoja atakatwa kiasi cha Sh2,850,000 kulingana na kanuni za maadili ambazo walisaini wakati wanaingia mikataba na timu hiyo.
Depu yuko nje kwa majeraha akiuguza nyama za paja akiwa kwenye hatua za kupona wakati Boka akiuguza maumivu ya kifundo cha mguu ambaye naye inaelezwa ameanza mazoezi ya gym akielekea kupona.
“Hatuna utani kwenye nidhamu, hao wachezaji kila mmoja anajua akifanya kosa ni adhabu gani itamkuta, nitakupa mfano kuna adhabu tumezitoa kwa wachezaji wawili, si unaona Depu anafanya vizuri lakini amepata adhabu kwa kosa la kutosafiri na timu,” amesema bosi huyo. “Kuna Boka naye amefanya kosa kama hilo hakusafiri na timu, unaweza kujiuliza kwanini tunawakata wakati ni majeruhi, hao wachezaji walitakiwa kusafiri na timu kwa kuwa majeraha yao yalitakiwa kusimamiwa na madaktari wetu ambao waliondoka na timu.
“Kila mmoja tumemkata gharama ya tiketi ya ndege lakini pia kosa hilo lina kiasi chake cha fedha na jumla kila mmoja atakatwa kiasi cha Sh2,850,000 kwenye mishahara yao na hili hatuna utani nalo, tunataka kila mchezaji kufuata maagizo ya klabu.
“Kuna wakati mliona Mzize (Clement) kabla ya kuumia kwa mara ya pili, alikuwa akisafiri na timu na huko tunakokweda wala alikuwa hachezi, achana na Mzize kuna Pacome (Zouzoua) naye tulikuwa tunakwenda naye Zanzibar na hakucheza mechi za huko, huu ni utaratibu wetu.
“Ukiacha suala la matibabu, lakini makocha wanaamini wachezaji hao hata kama hawafanyi mazoezi lakini wakikaa nje, watajifunza kile ambacho wenzao wanafundishwa uwanjani, hapo unawaondoa wale ambao watakaa nje kwa msimu mzima ndio pekee hawatakiwi kwenye safari zetu.”
Aidha Yanga pia itamchukulia hatua kinda mmoja kutoka kikosi chao cha vijana ambaye alionekana kucheza mashindano ya mpira wa miguu kipindi cha mfungo wa Ramadhan kutokana na kuzuiwa kwa wachezaji wao kucheza mashindano au mechi zisizo rasmi.
“Kuna kijana mwingine alionekana anacheza mashindano ya ndondo wakati wa mfungo wa Ramadhan, naye atakutana na adhabu yake, kama unaona hatupo makini basi huo ndio msimamo wetu,” amesema bosi huyo.
