Mechi nne kumpa mzuka Beimbaya B19 FC

WAKATI Ligi ya Championship ikisimama hadi Aprili 17, 2026 kwa ajili ya mzunguko wa 22, kocha wa timu ya B19 FC, Twaha Beimbaya amesema katika kipindi hiki anataka kukitumia vizuri kwa ajili ya kupata angalau mechi nne zenye ushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Beimbaya amesema hadi sasa wamepata mechi moja dhidi ya KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu huu japo mazungumzo na nyingine yanaendelea, ili kutumia vizuri kusahihisha changamoto tofauti zilizojitokeza.

“Lengo letu ni kutoka kabisa nafasi za kucheza mchujo ndio maana tunataka kupambana katika mechi zetu tisa zilizobakia, tunatambua ushindani ni mkubwa sana kutokana na malengo na mahitaji ya kila mmoja wetu,” amesema Beimbaya.

Beimbaya, amesema mechi hiyo na KMC ilitarajiwa kuchezwa jana Ijumaa, ingawa, uongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na benchi la ufundi wanaendelea kutafuta nyingine zaidi, ili Ligi itakaporejea, iwe rahisi kwao kuendana na ushindani huo.

“Ugumu uliopo unatokana na timu kutopishana gepu kubwa, kwa sababu mmoja akishinda anaweza kutoka nafasi ya 13 hadi ya 12, hivyo, ni lazima tucheze kwa tahadhari kubwa, hasa hizi mechi za mwishoni ambazo huwa ni ngumu,” amesema Beimbaya.

Kocha huyo aliyewahi kuifundisha Kiluvya United kwa sasa Barberian, amepewa jukumu la kukiongoza kikosi cha B19 zamani Tanesco kwa mkataba wa miezi sita, baada ya uongozi wa timu hiyo kuachana na Babou Salim kwa makubaliano ya pande mbili.

Beimbaya aliyewahi kuifundisha pia Pan Africans, kwa sasa ameiongoza B19 FC ikishika nafasi ya 12 na pointi 21, baada ya timu hiyo kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 10, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao 20 na kuruhusu 33.