Serikali yawabana wauzaji holela wa miwani za urembo

Dar es Salaam. Wakati ongezeko la wauzaji wa miwani ya urembo na fremu likishika kasi mitandaoni, Wizara ya Afya imetoa tahadhari juu ya hali hiyo, huku ikitaka udhibiti zaidi kufanyika ili kunusuru afya za Watanzania.

Ili kuzuia hilo, imependekezwa kwamba utoaji wa leseni za biashara za miwani, hata zile zinazoitwa za urembo ikiwemo ya jua, uambatane na cheti cha usajili kutoka Wizara ya Afya ili kuzuia wauzaji wasio na sifa kuuza bidhaa zinazoweza kuharibu uono wa watu.

Katika ukaguzi huo, wametembelea vituo vya huduma za macho 14, vikiwemo vile vilivyosajiliwa na vingine vilivyoanza kutoa huduma wakati vikiwa bado kwenye mchakato wa usajili.

Wametembelea wasambazaji 33 wa vifaa tiba kama fremu, lenzi tiba, na miwani ya jua, ambapo walibaini kuwa ni 10 pekee wenye ofisi rasmi na leseni, huku wengine 23 wakiwa wauzaji wa mitaani au machinga.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Baraza la Optometria kutoka Wizara ya Afya, Sebastiano Millanzi, jana, Machi 27, 2026 baada ya kufanyika kwa ukaguzi katika wilaya za Temeke, Kigamboni na Kinondoni, na kubaini kuwapo kwa ongezeko la watu wanaouza miwani tiba na lenzi kinyume na Sheria ya Optometria, jambo linaloweza kusababisha madhara kwa jamii.

“Kuna mgongano wa kimaslahi, jamii inaona miwani hiyo kama bidhaa za urembo, wakati kitaalamu ni vifaa vya matibabu. Baraza linasisitiza kuwa hakuna miwani ya urembo katika maana ya kawaida ya kibiashara, bali kila miwani ina kazi ya kitaalamu mwilini,” amesema.

Amesema tasnia ya magonjwa ya macho, neno “urembo” lina maana tofauti ambayo inamtaka mtaalamu kusoma umbo la sura na rangi ya mteja ili kumpa fremu inayomvutia na kuendana naye. Akitolea mfano, mteja mwenye ngozi nyeusi anaweza kushauriwa kutoivaa miwani yenye rangi nyeupe inayong’aa sana ili aendane nayo kitaalamu.

“Pia kuna hatari ya Contact Lenses za urembo. Tumebaini kuwa kuna watu wanachukua lenzi popote wanapojisikia kwa ajili ya urembo bila maelekezo ya kitaalamu, jambo ambalo ni hatari. Hii limeenda sambamba na miwani ya jua kwa ajili ya urembo bila kufanyiwa upimaji wa kina,” amesema na kuongeza:

“Ni hatari kwa sababu yanaweza kuficha dalili za ugonjwa wa presha ya macho, kwani mgonjwa anaweza kuhisi nafuu ya mwanga mkali anapovaa miwani hiyo na kuacha kwenda hospitali, huku ugonjwa ukiendelea kuharibu neva za macho kwa siri,” amesema.

Ili kukomesha suala hilo, walipendekeza utoaji wa leseni za biashara za uuzaji wa miwani, ikiwemo ya urembo na miwani ya jua, uambatane na cheti cha usajili wa kituo kutoka Wizara ya Afya ili kuhakikisha usalama wa jamii.

Mbali na uuzaji miwani holela, pia utafiti huo umebaini baadhi ya wataalamu wa optometria wanavuka mipaka ya kazi zao kwa kutibu magonjwa yanayohitaji rufaa kwa madaktari bingwa au kumiliki na kuuza dawa kinyume na taratibu.

“Kuna vituo vimeanza kutoa huduma bila kukamilisha usajili wa wizara, na kituo kimoja kilifungwa kwa kukosa mtaalamu na kutoa huduma zisizo za optometria,” amesema.

Amesema ni vyema kufanyika ufuatiliaji wa karibu kwa vituo vilivyokaguliwa ili kuvipa msaada wa kukamilisha usajili au kuvifunga kama havina sifa.

“Usimamizi wa takwimu za afya, kwani sasa kuna msisitizo mkubwa kwa vituo vyote kuanza kutumia na kujaza takwimu kwenye vitabu vya serikali (Mtuha). Hii itasaidia serikali kupata takwimu sahihi za matatizo ya macho ili kupanga bajeti na afua zinazostahili,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wafanyabiashara wa miwani ya urembo, Sheiba Kassim, amesema kabla ya hatua zozote kufanyika ni vyema wakapewa elimu ya kina, ili wafanye kazi zao kirahisi.

“Watuambie tufanye nini tusivunje sheria, kwani tunachokifanya sasa ni kuuza miwani isiyokuwa na lenzi ili kuwasaidia watu kupunguza mwanga wa jua au kompyuta,” amesema Sheiba.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Daktari Gunini Kamba, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, ameahidi kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa vituo vyote vilivyopitiwa ili kuona kama vimefanya marekebisho yaliyoelekezwa.

Pia, wataendelea kukagua vituo vingine ambavyo havikufikiwa katika awamu ya kwanza ya ukaguzi.

“Tutahakikisha kuwa mchakato wa usajili unafanywa kwa kasi kwa wamiliki wa vituo ambao tayari wanakidhi vigezo. Lengo ni kuhakikisha vituo vyenye sifa vinapata usajili wa baraza ndani ya muda mfupi ili kuondoa urasimu,” amesema.

Amesema wauzaji pia wa mitaani na wale wenye maduka wataendelea kupewa elimu ya sheria ya Optometria ili wafanye biashara zao kwa kufuata utaratibu wa kitaalamu.