Tiba mpya kuboresha via vya uzazi, urembo sehemu za siri

Dar es Salaam. Wakati wanawake wakikabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazohusiana na sakafu ya nyonga, matumaini mapya yanaanza kuonekana kupitia tiba za kisasa, inayohusisha huduma za kurekebisha na kuboresha via vya uzazi pamoja na urembo wa sehemu za siri.

Baadhi ya changamoto hizo zimekuwa zikiwafanya wanawake wenye uhutaji kutumia vilainishi kujitibu ukavu na uchafu ukeni, kupungua kwa hisia za kimapenzi, na maambukizi ya mara kwa mara au kutumia dawa zisizothibishwa kisayansi kubana uke huku wengine wakinywa antibaotiki kiholela.

Hayo yameelezwa Machi 25, 2026 na Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya CCBRT, Dk Said Suleiman alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu huduma hiyo.

Mbali na matibabu ya kiafya, Dk Suleiman ambaye ni mbobezi wa afya ya sakafu ya nyonga, amesema sasa kuna huduma za urembo wa sehemu za siri (vaginal aesthetics) ambazo zimeanza kupatikana nchini.

“Wanawake wengine wanakerwa na mabadiliko ya maumbile ya sehemu za siri, kama kulegea au kubadilika kwa ukubwa wa baadhi ya sehemu. Sasa tunaweza kurekebisha kulingana na mahitaji yao kwa njia salama na za kitaalamu,” amesema.

Ametahadharisha dhidi ya matumizi ya njia zisizo sahihi zinazotolewa mitandaoni au na watu wasio wataalamu, kama kutumia ndimu au vitunguu saumu, akisema zinaweza kuleta madhara na hazina ushahidi wa kisayansi.

“Wengine wanakerwa na ukubwa wa njia zao baada ya kujifungua au sasa anaona amekuwa na uke mpana.

“Huko nyuma kwa kuwa hakukuwa na taaluma, watu walikuwa wanafanya vitu visivyo sahihi, wanaambiwa waweke ndimu, vitunguu saumu, vipipi na vitu vingine ambavyo kitaalamu havipo na havijathibitishwa kama vinaweza kusaidia na kudumu kwa muda mrefu, lakini kitaalamu matibabu yamekuja ambayo yanaonekana yanasaidia,” amesema Dk Mohammed.

Katika kuimarisha mahusiano ya kimapenzi, amesema pia kuna tiba zinazolenga kuongeza msisimko kwa wanawake waliopoteza hamasa ya tendo la ndoa.

“Kuna wimbi kubwa la wanawake kupoteza hisia au kupungukiwa na wengi hawafurahishwi au hawafiki kileleni, kwa hiyo utaalamu nao umekuja na hiyo tiba.

“G spot ni sehemu maalumu ambayo humsisimua mwanamke, wakati mwingine inakuwa imefubaa haiwezi kufanya kazi vile ambavyo ilikuwa inatakiwa.

“Kwahiyo kuna sindano maalumu ndogo kabisa ambayo tunachoma ile sehemu inakwenda inasisimua na inarekebisha hii sehemu ya G Spot, ili akishiriki tendo na mwenza wake arudishe tena ule msisimko unaohitajika na sindano nyingine inaenda kuchomwa sehemu za kinembe, inaenda kumwongezea mishipa ya damu na fahamu kutengenezwa kwa wingi, hivyo kumwongezea msisimko sehemu ile,” amesema.

Dk Suleiman amesema fani hiyo bado ni mpya si tu nchini bali hata duniani, ilianza kujitokeza kuanzia mwaka 2008.

“Ukilinganisha na taaluma nyingine za tiba, hii bado iko katika hatua za mwanzo. Nchi nyingi za Afrika hazina wataalamu wa eneo hili. Tanzania tumeanza kuwa nao na mimi ni miongoni mwa waanzilishi,” amesema mtaalamu huyo aliyerejea nchini mwaka 2025.

Ameeleza baada ya kuwa daktari bingwa wa uzazi kwa miaka minne, aliongeza utaalamu kwa kusomea afya ya sakafu ya nyonga katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini, kwa miaka miwili zaidi.

Kwa mujibu wa Dk Suleiman, sakafu ya nyonga ni sehemu muhimu inayoshikilia viungo vitatu vikuu kwa mwanamke ikiwemo kibofu cha mkojo, via vya uzazi (ikiwemo mfuko wa uzazi na uke), pamoja na njia ya haja kubwa.

“Changamoto yoyote inayohusisha viungo hivi inaweza kuashiria tatizo la sakafu ya nyonga,” amefafanua.

Dk Suleiman amesema kadri umri unavyoongezeka, wanawake wengi huanza kupata matatizo kama kukojoa mara kwa mara, kushindwa kuzuia mkojo, au kuamka usiku kwenda chooni zaidi ya mara moja, hali ambayo mara nyingi huchanganywa na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).

“Wapo wanaotibiwa kama wana UTI sugu, lakini kumbe misuli ya sakafu ya nyonga imeanza kulegea. Bila uchunguzi sahihi, mtu anaendelea kutumia dawa ambazo hazihitajiki,” amesema.

Ameongeza hali ya mkojo kuvuja bila hiari, hasa wakati wa kukohoa au kubeba vitu vizito, si lazima iwe ni dalili ya uzee, bali udhaifu wa misuli hiyo unaosababishwa pia na mabadiliko ya homoni.

Mbali na hilo, amesema baadhi ya wanawake hupata maumivu makali chini ya tumbo au wakati wa kushiriki tendo la ndoa, hali ambayo mara nyingi hutibiwa kama ugonjwa wa PID bila uchunguzi wa kina.

“Wakati mwingine misuli ya sakafu ya nyonga hukakamaa na kusababisha maumivu makali. Hapa hakuna haja ya kutumia antibiotiki kama hakuna ushahidi wa maambukizi,” amesisitiza.

Changamoto nyingine kubwa ni ukavu wa uke, ambao umeongezeka kwa kasi na kusababisha wanawake wengi kukimbilia kutumia vilainishi vya dukani.

Amesema kabla ya kutumia vitu hivyo ni vema kwanza kupata uchunguzi kwa kuwa kuta za uke zina tabia ya kujitengeneza upya, hivyo kama kuna sababu imetokea shughuli ya kujitengeneza upya inasimama na ukavu unaanza.

“Ukavu wa uke unatokana na mambo mengi, ikiwemo kupungua kwa homoni, msongo wa mawazo na maambukizi ya mara kwa mara. Lakini sasa kuna tiba za kurejesha hali ya kawaida badala ya kutumia vilainishi kwa muda mfupi,” amesema.

Amesema, tiba hizo ni pamoja na dawa, sindano maalumu na mbinu za kisasa zinazosaidia kurejesha unyevunyevu wa uke kwa muda mrefu kwa kuchochea mwili kujitengeneza upya.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya wanawake wanakabiliwa na tatizo la kushuka kwa via vya uzazi, hali inayoweza kuanza hata kwa wasichana wadogo.

“Tumeona hata wasichana wa miaka 19 au 22 wakiwa na dalili za kushuka kwa kuta za uke. Lakini wengi hukaa na hali hii kwa muda mrefu kutokana na aibu au kukosa uelewa,” amesema.

Dalili zake ni pamoja na kuhisi uzito sehemu za siri, maumivu ya tumbo la chini, au kuhisi kitu kisicho cha kawaida ndani ya uke.

Dk Suleiman amesema matibabu yapo, kuanzia mazoezi maalum hadi upasuaji mdogo wa kurekebisha hali hiyo.

Katika eneo la haja kubwa, amesema baadhi ya wanawake hupata tatizo la bawasiri au kushuka kwa kuta za njia ya haja kubwa, hali inayoweza kuathiri maisha ya kawaida na hata mahusiano.

Pia, amegusia changamoto za watoto wanaozaliwa na hitilafu za maumbile ya via vya uzazi, akisema upasuaji wa kurekebisha unafanyika na kuwasaidia kuishi maisha ya kawaida.

Kwa upande wa tatizo la uchafu ukeni, Dk Suleiman amesema: “Kuna changamoto ambayo kwa sasa imekuwa zaidi, wanawake wanapambana na uchafu wa rangi kama ya maziwa, kijani, njano, kama damu ya mwezi, maziwa mgando na mwingine una harufu kali au hauna harufu; baadhi ukitoka wanawashwa ukeni wengine hawawashwi, changamoto ya hili tatizo wengi wanajitibia wenyewe, anaenda duka la dawa tu.”

Amesema hali hiyo imesababisha kutengenezwa wadudu sugu wa dawa zinazotumika mara kwa mara, anapona siku mbili, ile hali inarudi tena.

“Tunashauri kabla hujapata matibabu nenda ukamuone daktari wa kinamama achukue ule uchafu na kuuotesha maabara, lengo kumuua yule bakteri husika, la sivyo bakteria wale hupanda juu na kwenda kuathiri via vya uzazi na ndiyo inakua PID ambayo inaharibu shingo ya uzazi, mirija na mayai ya uzazi na kusababisha madhara makubwa ikiwemo ugumba,” amesema Dk Suleiman.

Katika hatua nyingine, CCBRT imeandaa kambi maalumu ya matibabu ya bure kwa wanawake wenye changamoto za sakafu ya nyonga.

Kambi hiyo itafanyika Machi 30 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni katika jengo la mama na mtoto, Msasani, Dar es Salaam.

“Tunawahimiza wanawake wote wenye dalili kama kushindwa kuzuia mkojo, maumivu ya nyonga, kushuka kwa via vya uzazi au changamoto za kimapenzi kujitokeza kupata huduma hii muhimu bila malipo,” amesema.

Ameongeza kuwa lengo ni kuongeza uelewa na kuhakikisha wanawake wanapata matibabu sahihi mapema badala ya kuendelea kuishi na matatizo yanayoweza kutibika.

Baadhi ya wanawake wametoa maoni yao kuhusu huduma hiyo, wakisema huenda ikawa mkombozi kwa maana changamoto za maradhi ya sakafu ya nyonga yanawasumbua wengi.

“Kwa muda mrefu wanawake tumekuwa tukinyamaza kuhusu matatizo ya sehemu za siri kwa sababu ya aibu na hofu ya kuhukumiwa. Lakini ukweli ni kwamba changamoto hizi zinaathiri sana afya na hata mahusiano yetu. Kusikia kuwa kuna tiba za kisasa zinazoweza kusaidia, kunatupa matumaini mapya ya kuishi maisha ya kawaida bila usumbufu,” amesema Rebeca Osward, mkazi Dar es Salaam.

Hata hivyo wanaume wamesema huchukulia baadhi ya hali kama kupungua kwa hamasa ya tendo la ndoa kuwa ni tatizo la kawaida au la kimahusiano tu, lakini kama tiba zikipatikana itaokoa mahusiano yao.

“Kwa upande wetu wanaume, mara nyingi hatuelewi changamoto wanazopitia wanawake kwenye afya ya sehemu za siri. Lakini ukweli ni kwamba matatizo haya yanaathiri hata mahusiano. Elimu zaidi inahitajika ili tuweze kuwaunga mkono wenza wetu badala ya kuwahukumu,” amesema mkazi wa Morogoro, Alfred Lyimo.