Geita. Wahudumu wa afya mkoani Geita wametakiwa kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kwa umma pamoja na kuzingatia ukusanyaji sahihi wa takwimu kuhusu ugonjwa wa hemophilia, ili kuimarisha mwitikio wa wananchi kupima na kuanza matibabu mapema wanapogundulika kuwa na changamoto hiyo.
Hemophilia ni ugonjwa unaosababisha damu kushindwa kuganda kwa urahisi, hivyo mhusika hupoteza damu nyingi anapopata jeraha.
Hali hiyo husababishwa na upungufu wa baadhi ya chembechembe muhimu za damu. Takwimu za dunia zinaonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10,000 huathirika na ugonjwa huo, huku asilimia 70 ya wagonjwa wakiwa wameurithi.
Rai hiyo imetolewa Machi 27, 2026, na Kaimu Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Hemophilia nchini, Abdallah Makala, wakati wa uzinduzi wa kliniki ya ugonjwa huo mkoani Geita, ulioambatana na semina kwa wahudumu wa afya na maofisa elimu.
Makala amesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu na utunzaji sahihi wa takwimu, akieleza kuwa upungufu wa taarifa sahihi unaweza kusababisha wagonjwa kukosa dawa katika maeneo husika.
“Tuongeze kasi ya utoaji elimu na kukusanya takwimu sahihi. Wagonjwa wanaweza kukosa dawa kwa sababu taarifa hazijakusanywa au kuwasilishwa kwa wakati,” amesema.
Makamu Mwenyekiti Chama cha Hemophilia nchini, James Seye akizungumza katika semina ya kuwajengea uelewa watalamu wa afya kuhusu ugonjwa huo mkoani Geita.
Amebainisha kuwa Tanzania, takribani wagonjwa 6,700 wanakadiriwa kuishi na hemophilia, lakini ni wagonjwa 600 pekee waliogundulika na kuanza matibabu, hali inayoonesha uhitaji mkubwa wa kuongeza uelewa kwa jamii.
Kliniki hiyo imeanzishwa kwa ufadhili wa Novo Nordisk Haemophilia Foundation kwa kushirikiana na World Federation of Hemophilia, ikiwa na lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kuboresha ukusanyaji wa takwimu. Mpango huo pia unatarajiwa kupanuliwa katika mikoa ya Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Lindi na Singida.
Kupitia mradi huo mkoani Geita, zaidi ya Sh5.6 milioni zimetolewa kwa ajili ya vifaa na vitendanishi vya maabara, huku zaidi ya Sh525 milioni zikitumika kununua dawa kwa ajili ya wagonjwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Omari Sukari, amesema gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja zinaweza kufikia hadi Sh200 milioni kwa mwaka, jambo linalofanya ufadhili huo kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kipato cha kawaida.
Ameongeza kuwa ugonjwa huo huathiri zaidi wanaume, ingawa wanawake pia wanaweza kuugua. Hadi sasa, wagonjwa sita wamegundulika mkoani Geita.
Amewataka wataalamu waliopata mafunzo kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa na kuwahamasisha wananchi kufika katika vituo vya afya kupata huduma.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Hemophilia nchini, James Seye, ameshauri kuboreshwa zaidi kwa huduma kwa wagonjwa hao, ikiwamo kuwashirikisha katika utoaji wa elimu kwa kuwa wana uzoefu wa moja kwa moja wa changamoto wanazokutana nazo.
Kwa upande wake, Mgeza Mihina, ambaye ni mgonjwa wa Hemophilia A na pia mtaalamu wa maabara, amesema ukosefu wa uelewa katika jamii umekuwa changamoto kubwa, hususan katika ajira, ambapo baadhi ya waajiri huonesha wasiwasi kuwaajiri kutokana na hali zao za kiafya.
Amesisitiza kuwa, pamoja na kufunguliwa kwa kliniki, bado kuna haja ya kuimarisha utoaji wa elimu na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa wakati ili kuokoa maisha ya waathirika wa ugonjwa huo.
