TASAF YAUNGA MKONO SERIKALI UBORESHAJI HUDUMA YA AFYA, YATOA MSAADA OCEAN ROAD

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Maendeleo ya jamii(TASAF)umeunga mkono juhudi za Serikali katika huduma ya afya kwa kutoa msaada muhimu katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Msaada huo umekabidhiwa leo hospitalini hapo na Meneja rasilimali watu wa mfuko huo Mariam Al- Jabiri kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray.

Al Jabir ambaye ameambatana na baadhi ya wafanyakazi wa Tasaf amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini.

“Msaada huu umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini,”amesema huku akiwatakia uponyaji wa haraka wagonjwa wote wanaopata matibabu katika taasisi hiyo.

Aidha baadhi wa Wafanyakazi hao wa TASAF wakiongozwa na Meneja huyo wamepata nafasi ya kuwajulia hali wagonjwa hospitalini hapo huku wakiwafariji kwa kuwatia moyo na kufanya sala fupi kuwaombea uponyaji wa haraka.

Kwa upande wake Mwakalishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Road Dk.Diwani Msemo ameushukuru mfuko wa maendeleo ya jamii kwa msaada huo.