Dar es Salaam. Wizi wa vifaa vya ujenzi umeanza kuwa tatizo linaloongezeka katika baadhi ya maeneo ya makazi, hasa katika maeneo ambayo ujenzi huchukua muda mrefu kukamilika.
Katika mazingira hayo, wahusika wa wizi hutumia mwanya wa kutokuwepo kwa uangalizi wa karibu wa mara kwa mara kuiba vifaa vyenye asili ya chuma.
Wizi huu kwa kiasi kikubwa unashirikisha wauzaji wa vyuma chakavu kwa sababu wao ndiyo wanunuzi wa vitu hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi na mafundi, wizi huo mara nyingi hufanyika kwa siri, hususan nyuma ya nyumba zinazojengwa au katika maeneo ambayo hayapo wazi kwa macho ya watu wengi.
Katika baadhi ya matukio, nondo zinazotokeza kwenye zege au nguzo (matoleo) hukatwa na kuchukuliwa usiku bila mwenye nyumba kugundua.
Mbinu hiyo imekuwa ikiwafanya baadhi ya wamiliki wa majengo kugundua hasara hiyo baada ya muda mrefu, hali inayoongeza gharama za ujenzi na kuchelewesha kukamilika kwa nyumba zao.
Wamiliki wa majengo yanayoendelea kujengwa wameibuka na kilio kizito wakieleza namna wanavyopata hasara kubwa kutokana na wizi wa vifaa vya ujenzi, wakisema hali hiyo imekuwa ikichelewesha miradi yao na kuongeza gharama zisizokuwa kwenye mipango yao ya awali.
Wengi wao wanasema wanapanga bajeti ya ujenzi kwa kuzingatia hatua kwa hatua, lakini wanajikuta wakilazimika kurudia kununua vifaa walivyokwisha kununua kutokana na kuibiwa, jambo linalowarudisha nyuma kifedha na kisaikolojia.
Mkazi wa Sinza, Nassoro Mansour ambaye anajenga nyumba yake Kigamboni anasema alikumbana na tukio la kukatwa kwa nondo zilizokuwa zimetokeza kwenye nguzo (matoleo), hali iliyomuumiza kwa kiasi kikubwa.
“Nilipofika siku hiyo nilikuta nondo zimekatwa kwenye kibaraza cha nyuma na baadhi ya vyumba. Niliumia sana kwa sababu inanibidi kununua nondo nyingine na kulipa mafundi upya, na hapa gharama zimeongezeka maradufu,” anasema Mansour.
Naye, Emmanuel Nehemia anayejenga Goba, anasema wezi walikata kitasa cha geti na kuingia ndani kisha kuiba nyaya zote alizokuwa ametandaza ndani ya nyumba na kumuachia mabomba.
“Niliibiwa nyaya za nyumba nzima ambazo gharama zake zilikuwa zaidi ya Sh 1 milioni, na nilikuwa natarajia kuhamia mwezi mmoja baada ya kukamilisha hilo, ndiyo maana sikuweka mtu wa kulinda,” anasema.
Wakati hao wakilalamika hivyo, Rose Kimario anasema aliibiwa madirisha matatu katika nyumba yake ya Msongola kabla hayajakauka, na aligundua siku ya pili alipokwenda kuiangalia.
“Nikimkuta mwizi anapigwa natupia hata jiwe. Niliibiwa madirisha yangu yakiwa mabichi; sitamani hata kukumbuka, maana hadi naondoka jioni yalikuwepo yote, lakini siku inayofuata mchana matatu hayapo,” anasema Rose.
Fundi ujenzi ameibuka na kueleza namna wizi wa nondo na vifaa vingine unavyowaathiri moja kwa moja katika utekelezaji wa kazi zao, akisema hali hiyo inawalazimu kufanya kazi ya ziada ambayo haikuwa sehemu ya makubaliano ya awali na mteja.
Fundi ujenzi kutoka Kinyerezi, Hamad Omari, anasema kila fundi anapopokea kazi huwa tayari ameweka makadirio ya vifaa na gharama kulingana na mchoro wa jengo, lakini wizi unapojitokeza hulazimika kubadili mpango huo.
Kwa mujibu wa fundi, kila hatua ya ujenzi hupangwa kwa kuzingatia vipimo, gharama na muda maalum wa utekelezaji. Hivyo, nondo zinapokatwa au kuibiwa baada ya kazi fulani kukamilika, hulazimika kurudi nyuma na kuanza upya katika baadhi ya maeneo, jambo linalovuruga mpangilio mzima wa kazi.
“Kila fundi anapojenga anakuwa na hesabu zake. Nondo zinapokatwa, inamaanisha kuna kazi mpya imejitokeza ambayo haikuwa kwenye makubaliano ya mwanzo,” anasema.
Anasema hulazimika kutindua sehemu za zege zilizokuwa tayari zimekamilika ili kuweka nondo mpya, hatua ambayo si tu inaongeza kazi bali pia inahitaji umakini mkubwa ili kulinda uimara wa jengo.
“Nondo zikishakatwa, tunalazimika kutindua sehemu ya zege ili kuweka nyingine. Si kazi rahisi; inaanza kufikirisha upya hesabu za ujenzi, inachukua muda na inaongeza gharama kwa mwenye nyumba,” anaeleza Omari.
Aidha, Omari anaonya kuwa endapo marekebisho hayo hayatafanywa kwa umakini na utaalamu wa kutosha, yanaweza kuathiri ubora na usalama wa jengo kwa muda mrefu.
“Wakati mwingine ubora wa jengo unaweza kuathirika kama kazi haikufanywa kwa umakini mkubwa. Hii ni kwa sababu unakuwa unarekebisha kitu ambacho tayari kilikuwa kimeanza kukomaa,” anasisitiza.
Fundi huyo anashauri wamiliki wa majengo kuhakikisha wanakuwa na ulinzi wa uhakika katika maeneo ya ujenzi ili kuepusha hasara zinazoweza kuzuilika pamoja na kulinda ubora wa majengo yao.
Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za Mtaa mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Mwingamno, anasema wizi wa vifaa vya ujenzi unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji unatokana na mchanganyiko wa changamoto za ulinzi, mazingira ya maeneo mapya ya makazi pamoja na uzembe wa baadhi ya wamiliki wa majengo.
Anasema maeneo yanayoathirika zaidi ni yale yaliyo nje kidogo ya mji au yanayoendelea kukua kwa kasi, ambapo bado hayajawa na makazi ya kudumu na mifumo imara ya ulinzi.
“Maeneo mengi yanayoendelea kujengwa yako pembezoni mwa mji; hayajakaa vizuri. Watu wanajenga lakini hawaishi hapo, hivyo yanakuwa rahisi kwa wezi kufanya uhalifu bila kugundulika,” anasema Mwingamno.
Katika mazingira hayo, anasema hata ulinzi shirikishi unakuwa na mipaka, hasa pale ambapo hakuna wakazi wa kudumu au michango ya kugharamia ulinzi huo.
“Ulinzi shirikishi unategemea ushirikiano wa wananchi. Sasa kama eneo halina watu wanaoishi au kulipia ulinzi, inakuwa ngumu sana kulinda. Licha ya jitihada za ulinzi, bado ni vigumu kubaini wahusika wa wizi huo kwa urahisi kutokana na mbinu wanazotumia.”
Anasema mwizi haibi mbele ya macho; atavizia nyuma ya jengo, na kwa maeneo mengi ambayo bado hayajajengwa, ni vigumu kumtambua kwa macho ya kawaida.
Pia, Mwingamno anagusia uwezekano wa baadhi ya watu waliopo karibu na miradi hiyo kuhusika, ikiwemo mafundi au watu wanaofahamu muundo wa jengo.
“Wakati mwingine si rahisi kusema nani anahusika moja kwa moja, lakini kuna uwezekano hata wa watu wanaojua mfumo wa jengo, kama mafundi, kujua sehemu gani ni rahisi kuchukua na kurudi kuiba,” anasema Mwingamno.
Kutokana na hali hiyo, amewashauri wamiliki wa majengo kuchukua hatua binafsi za kujilinda badala ya kutegemea ulinzi shirikishi pekee.
“Kama umefikia hatua ya kuweka wiring au vifaa vya thamani, ni lazima uweke mtu wa kulinda. Hauwezi kuacha mali zako wazi halafu utegemee ulinzi wa nje pekee.”
Hata hivyo, anasema serikali za mitaa zinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulinzi wa mali zao, huku juhudi za kuimarisha ulinzi zikiendelea kufanyika.
“Sisi kama viongozi tunaendelea kusisitiza masuala ya ulinzi na usalama, lakini ni muhimu kila mmoja akachukua hatua za kulinda mali zake ili kupunguza matukio haya,” anasema Mwingamno.
Akizungumza na Mwananchi Machi 20, 2026, Kamanda wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro, anasema jambo linalofanyika halikubaliki kwa jamii inayojitafuta na linarudisha nyuma maendeleo yao.
“Wizi huu si sawa na hatuwezi kukubaliana nao. Naomba nichukue suala hili kwa ajili ya kufanyia kazi, kwani halikubaliki hata kidogo na linahatarisha maisha ya watu katika kuweka uimara wa jengo,” anasema Muliro.
